Dkt. Homera Aridhishwa RITA Kuwajengea Uwezo Wadhamini Katika taasisi ili kuepusha migogoro

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Juma Zuberi Homera afungua Mkutano WA wajumbe amefurahishwa na mpango wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kuendelea kutoa elimu na kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi za Wadhamini kutoka taasisi mbalimbali ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza katika kuziendesha taasisi zao.
Akizungumza wakati wa Mkutano ambao umefanyika Dodoma Dkt.Homera ameipongeza Rita kwa juhudi ambazo wanazifanya kwa kuendelea Kuwajengea Uwezo,wajumbe wa Bodi za Wadhamini kutoka taasisi mbalimbali ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza Katika kuziendesha taasisi zao.
“Nawashukuru Rita kwa kunialika ili kufungua Mkutano huu muhimu sana wa wajumbe wa bodi za wadhamini zilizopo mikoa ya Dodoma, Morogoro, Singida, Iringa na Manyara kwa ajili ya kuwajengea uwezo kusimamia taasisi zao,” amesema.
“Bodi za Wadhamini ni nguzo muhimu katika ustawi wa taasisi zisizo za kiserikali, taasisi za kidini, michezo, na taasisi nyingi zinazotoa huduma mbalimbali kwa jamii.

Amesema mkutano huo ni muhimu kwani utawezesha kupunguza au kumaliza kabisa changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya bodi za wadhamini na hivyo kuziathiri taasisi wanazozisimamia.
“Pamoja na mafanikio yaliyopatikaa, bado ipo changamoto ya baadhi ya bodi za wadhamini kutotimiza majukumu yao kikamilifu kwa kutumia mali za taasisi kwa maslahi binafsi, kufanya ubadhirifu wa mali na fedha, kujimilikisha mali kinyume cha utaratibu, Bodi za Wadhamini kukaa madarakani zaidi ya muda ulioainishwa katika Katiba hivyo kusababisha migogoro na uvunjifu wa amani.
Hata hivyo ameipongeza RITA kwa hatua mbalimbali inazochukua kwa lengo la kutatua na kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika Bodi za Wadhamini.
“Hakika haya ni mageuzi makubwa yanayoendana na wakati tuliopo ambao bila matumizi ya mifumo ya kidijitali taasisi haiwezi kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wadau wake,” amesema Dkt.Homela.
Aidha, Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Bw. Frank Kanyusi ameweka wazi kwamba Wadhamini wamepewa mamlaka na kuaminiwa kusimamia mali za Taasisi kwa faida ya wanachama au wanufaika kulingana na madhumuni ya kuanzishwa taasisi husika kama yalivyoainishwa katika katiba.
Amesema kuwa taasisi hiyo inakusudia kuanzisha huduma za “mobile Clinics” kwa lengo la kutoa ushauri, kutatua changamoto papo kwa papo, na kusogeza huduma karibu na wadau.
Bw. Kanyusi amesema kuwa Usajili wa Bodi ya Wadhamini ni hatua muhimu kwani inaipa taasisi na utu wa kisheria wa kumiliki mali, kuingia mikataba kwa niaba ya Taasisi, kushitaki au kushitakiwa niaba ya Taasisi.
“Utaratibu huu unaongozwa na Sheria ya Usajili wa Bodi za Wadhamini Sura ya 318 toleo la 2002. (The trustees’ Incorporation Act CAP 318 R.E. 2002) amesema.

