Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, ameipongeza Bodi na Menejimenti ya Benki ya TCB kwa mikakati madhubuti iliyolenga kuboresha na kuimarisha utendaji wa benki hiyo.
Akizungumza Desemba 3, 2025 katika hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya TCB (TCB Stawi Bond) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, CPA Mkama alisema uamuzi wa benki hiyo kutoa hatifungani kwa umma umeongeza mtaji na kukuza fursa za uwekezaji katika masoko ya mitaji, jambo linalochangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Hatifungani ya TCB iliidhinishwa chini ya Sheria na Kanuni za Masoko ya Mitaji na imepata mafanikio makubwa katika mauzo, ikiwa imeuzwa kwa asilimia 281 ya malengo. Benki ilikusanya shilingi bilioni 140.24 dhidi ya shilingi bilioni 50 zilizotarajiwa. Mafanikio haya yanaiwezesha TCB kuongeza ukwasi, kuimarisha mtaji wake na kupanua huduma kwa wananchi na wajasiriamali.
TCB imeweka historia kuwa benki ya kwanza inayomilikiwa na Serikali kwa kiwango kikubwa cha hisa kuuza hatifungani kwa umma na kupata mafanikio makubwa, hatua inayofungua milango kwa taasisi nyingine za umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kuendesha miradi ya maendeleo.
Hatua hii pia ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Serikali wa Njia Mbadala za Kugharamia Miradi ya Maendeleo na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30.
CPA Mkama alieleza kuwa kati ya wawekezaji, asilimia 96.7 ni wawekezaji mmoja mmoja na asilimia 3.3 ni kampuni na taasisi. Aidha, asilimia 99.6 ni wawekezaji wa ndani. Kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo kumeongeza thamani ya uwekezaji wa hatifungani za kampuni na taasisi hadi kufikia shilingi trilioni 1.8 kutoka trilioni 1.7.



.jpeg)
.jpeg)
