The House of Social Media
gunners X

Trump Aipa Iran Onyo, Atishia Mashambulizi Endapo Waandamanaji Watadhuriwa

0
Rais wa Marekani, Donald Trump

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameitoa onyo kali kwa serikali ya Iran, akitishia kuishambulia nchi hiyo kwa “nguvu kubwa” endapo itatumia silaha dhidi ya wananchi wake wanaoendelea na maandamano makubwa ya kudai mabadiliko.

Akizungumza katika mahojiano maalum na mtangazaji wa Fox News, Sean Hannity, ndani ya Ikulu ya White House, Rais Trump amesema kuwa Iran imewekwa chini ya uangalizi maalum wa Marekani kufuatia hali ya kisiasa inayotikisa taifa hilo.

Trump amesema Marekani iko tayari kuchukua hatua kali za kijeshi iwapo utawala wa Iran utaanza kuwapiga risasi waandamanaji, ambao amewataja kuwa ni raia wasio na silaha wanaopigania mustakabali wa nchi yao.

“Nimewatahadharisha wazi. Wakifanya jambo lolote baya kwa watu hawa, tutawapiga kwa nguvu sana. Hawa ni watu wasio na silaha kabisa. Wanataka mabadiliko yatokee; nchi yao imerudi nyuma kwa zaidi ya miaka 150,” amesema Rais Trump.

Kauli hiyo imekuja wakati Iran ikishuhudia wimbi la maandamano katika miji mbalimbali, yakichochewa na hasira za wananchi kuhusu hali ya uchumi, uhuru wa kisiasa na haki za binadamu.

Onyo la Trump linaashiria kuongezeka kwa mvutano kati ya Marekani na Iran, huku jumuiya ya kimataifa ikiendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa maandamano na hatua zitakazochukuliwa na serikali ya Tehran.

 

Leave A Reply