The House of Social Media
gunners X

Polisi Wafanya Uchunguzi wa Matukio Matatu ya Vifo Tarime-Rorya, Arusha na Rufiji

0

Jeshi la Polisi Tanzania linafanya uchunguzi wa kina kuhusiana na matukio matatu ya vifo yaliyotokea kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Tarime/Rorya, Jijini Arusha na Wilayani Rufiji.

Tukio la kwanza linahusu kifo cha Dickson Tadeus Joseph, mkazi wa Rebu Senta Wilayani Tarime, kilichotokea tarehe 1 Januari, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime. Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limepokea barua ya malalamiko ikieleza kuwa kifo hicho hakikusababishwa na marehemu kuanguka katika eneo la Mtaa wa Serengeti wakati akikimbia, kama ilivyoelezwa awali, bali kinadaiwa kusababishwa na Askari Polisi.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina, na iwapo ushahidi kutoka kwa mashuhuda utabainisha kuwa kuna Askari aliyehusika, hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Tukio la pili linahusu kifo cha Viollete Uwumuhoza, raia wa Rwanda, aliyefariki dunia tarehe 7 Januari, 2026 baada ya kujinyonga akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Jijini Arusha. Marehemu alikuwa akishikiliwa kwa kosa la kuingia na kuishi nchini kinyume cha sheria. Uchunguzi wa kina unaohusisha mbinu za kisayansi na uchunguzi wa haraka unaendelea ili kubaini chanzo na mazingira ya tukio hilo.

Sambamba na matukio hayo mawili, Jeshi la Polisi linamshikilia Askari mmoja wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji kwa tuhuma za kumpiga risasi Shaban Said Luluba, mkazi wa Kijiji cha Nyamwage Wilayani Rufiji, wakati wa zoezi la ukamataji lililofanyika tarehe 8 Januari, 2026, tukio lililopelekea kupoteza maisha kwa raia huyo.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, na iwapo itabainika kuwa kulikuwa na uzembe au matumizi ya nguvu kupita kiasi, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya Askari huyo.

Jeshi la Polisi linaendelea kusisitiza dhamira yake ya kusimamia sheria, haki na uwajibikaji kwa wote bila upendeleo.


Imetolewa na:
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi
Dodoma, Tanzania

Leave A Reply