CAF Yafuta Michuano ya CHAN, Mabadiliko Makubwa Yatarajiwa Afrika

Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetangaza rasmi kufutwa kwa Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), kufuatia changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika maandalizi na uendeshaji wa mashindano hayo.
Uamuzi huo umetangazwa na Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika nchini Morocco siku ya Jumamosi, Januari 17. Motsepe amesema kuwa baada ya tathmini ya kina, imebainika kuwa CHAN imekuwa ikikabiliwa na matatizo ya mara kwa mara ambayo yameathiri ubora na ufanisi wa mashindano hayo.
Ameeleza kuwa CAF haiwezi kuendelea kusimamia mashindano ambayo hayakidhi viwango vya juu vya ushindani, maandalizi na uendeshaji wa kitaalamu vinavyotarajiwa na wadau wa soka barani Afrika.
Kwa mujibu wa Motsepe, kufutwa kwa CHAN ni sehemu ya mabadiliko makubwa yanayolenga kuifanyia marekebisho kalenda ya soka Afrika. Amebainisha kuwa mashindano mapya yanatarajiwa kuanzishwa ili kuchukua nafasi ya CHAN, yakiwa na lengo la kuinua kiwango cha soka na kutoa fursa bora zaidi kwa maendeleo ya vipaji barani Afrika.
Aidha, Rais huyo wa CAF amesisitiza kuwa shirikisho hilo litaendelea kufanya maamuzi kwa uhuru wake, huku likidumisha ushirikiano na mashirika ya soka duniani kwa kuzingatia maslahi ya maendeleo ya soka la Afrika.
Uamuzi wa kufuta CHAN unatarajiwa kuzua mjadala mpana miongoni mwa wadau wa soka, hususan kuhusu mustakabali wa wachezaji wanaocheza katika ligi za ndani na nafasi zao katika mashindano ya kimataifa.

