
Wanafunzi 13 wamefariki dunia nchini Afrika Kusini baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kugongana na lori kusini mwa jiji la Johannesburg. Ajali hiyo ilitokea Jumatatu asubuhi majira ya saa 1:00 kwa saa za huko (05:00 GMT) katika eneo la Vanderbijlpark, kwa mujibu wa mamlaka ya elimu ya eneo hilo.
Wanafunzi 11 walifariki papo hapo katika eneo la ajali, huku wawili wakifariki baadaye kutokana na majeraha waliyoyapata. Aidha, wanafunzi wengine wawili wameripotiwa kuwa katika hali mbaya mahututi, huku madaktari wakijitahidi kutoa matibabu.
Msemaji wa polisi, Mavela Masondo, alisema kuwa dereva wa basi hilo dogo amekiri kugonga lori baada ya kujaribu kupita magari mawili kwa wakati mmoja. Masondo aliongeza kuwa kesi ya mauaji yasiyokusudiwa itafunguliwa ili kuchunguza ajali hiyo kwa kina.
Idara ya elimu ya mkoa wa Gauteng imesema kuwa dereva wa basi anapatiwa matibabu hospitalini, huku taarifa kuhusu hali ya dereva wa lori zikiwa bado hazijabainika. Hali hii imezua wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa usafiri wa wanafunzi katika eneo hilo.
Ajali za barabarani zinazosababisha vifo ni za kawaida nchini Afrika Kusini, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo mwendo wa kasi kupita kiasi, uendeshaji hatarishi wa magari na magari yasiyotunzwa ipasavyo. Mwaka 2025 pekee, watu 11,418 walifariki kutokana na ajali za barabarani, idadi ambayo ni pungufu kwa takribani asilimia 6 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, lakini bado ni sawa na wastani wa vifo 31 kwa siku

