Kilimo Viwanda Jinsi Elimu Inavyobadilisha Sekta Ya Kilimo Tanzania
Dunia inapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Elimu, mjadala unaelekezwa kwenye nafasi ya elimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania. Kilimo kinaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, hata hivyo sekta hii inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ukosefu wa wataalamu wa kutosha na fursa chache za elimu kwa vijana, hasa wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini. Aidha, wakulima wengi wa vijijini hukosa msaada wa kitaalamu unaohitajika ili kuongeza tija na kuendana na kilimo cha kisasa.Changamoto hizi ndizo zilizochochea kuanzishwa kwa Programu ya Kilimo Viwanda mwaka 2020. Programu hii ni matokeo ya ushirikiano kati ya taasisi nne za mafunzo ya kilimo na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), ikilenga kuwawezesha vijana kutoka familia zenye uhitaji kupata elimu ya stashahada katika masomo ya kilimo. Hadi sasa, zaidi ya wanafunzi 300 wamenufaika na programu hii katika kipindi cha miaka mitano, wanafunzi ambao wengi wao wasingeweza kuendelea na masomo yao bila msaada huo.

Ushirikiano kati ya SBL na vyuo vya mafunzo ya kilimo ulikuwa wa kimkakati. Kabla ya kuanzishwa kwa programu, vyuo hivyo vilikabiliwa na changamoto ya wanafunzi wengi kukatisha masomo kutokana na kushindwa kumudu gharama za ada. Hali hii ilisababisha upungufu wa wataalamu wa ugani wa kilimo, ambao ni kiungo muhimu katika kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji. Kupitia ushirikiano huu, SBL imechangia kuongeza uhakika wa wanafunzi kuendelea na masomo, kuimarisha uwezo wa taasisi za elimu, na kuhakikisha mafunzo ya kilimo yanaendana na mahitaji halisi ya sekta.
Programu ya Kilimo Viwanda pia inaendana kikamilifu na vipaumbele vya kitaifa vya maendeleo. Kwa kuongeza idadi ya wataalamu wa kilimo na kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo, programu hii inachangia juhudi za Serikali katika kuboresha uzalishaji wa kilimo, kuimarisha usalama wa chakula, na kukuza kilimo cha kibiashara.

Ushirikiano huu unaunga mkono mikakati ya kitaifa ya kuiboresha sekta ya kilimo na kuimarisha viwanda vya ndani.
“Kilimo Viwanda ilianzishwa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wenye uwezo hawanyimwi fursa ya elimu ya kilimo kwa sababu ya changamoto za kifedha, huku ikijibu pia upungufu wa maafisa ugani wanaohitajika kuwahudumia wakulima kote nchini,” anasema, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Kilimo Igabiro, Muleba – Kagera, Sadock Stephano.
Kupitia programu hii, rasilimali watu katika sekta ya kilimo imeimarishwa kwa kiasi kikubwa. Wahitimu wake sasa wanafanya kazi kama maafisa ugani, wajasiriamali wa kilimo, na wasimamizi wa mashamba, wakichangia kuongeza tija kwa wakulima, kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa, na kuimarisha kilimo cha kibiashara.

Kwa upande wa Kampuni ya Bia ya Serengeti, programu hii inaakisi dhamira ya kampuni katika kuchangia maendeleo ya taifa na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa malighafi za ndani. “Kilimo Viwanda ilianzishwa ili kuwasaidia wakulima wanaozalisha mazao muhimu kama mahindi, shayiri na mtama kwa kuimarisha ujuzi wa kilimo, kuongeza uzalishaji, na kupanua fursa za masoko ya mazao yanayolimwa hapa nchini,” anasema, Meneja Mwandamizi – Mawasiliano na Uendelevu wa Kampuni ya Bia ya Serengeti Rispa Hatibu.
Kwa wanufaika, athari za programu zimekuwa za mabadiliko makubwa ya maisha. Khadija Msuguru, mmoja wa wahitimu wa programu hiyo, anasema ufadhili alioupata ulimpa fursa ya pili ya kutimiza ndoto zake. “Kabla ya kupata ufadhili, nilikuwa karibu kukata tamaa kuendelea na masomo kwa sababu ya kukosa ada. Leo, ninaendesha biashara ya usanifu wa mandhari na bustani, nikitumia ujuzi nilioupata kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine,” anasema.
Mnufaika mwingine, Octavian Burchard, anaendelea kutumia maarifa aliyopata ndani na nje ya mazingira ya darasani, akisimamia shamba la chuo chake huku akijihusisha na uzalishaji wa mazao kwa ajili ya viwanda. “Kilimo Viwanda kimenifanya nione kilimo kama biashara na daraja la kuelekea kwenye viwanda. Lengo langu ni kuzalisha mazao yanayokidhi viwango vya viwandani na kuchangia ongezeko la thamani katika sekta ya kilimo,” anasema.
Kadri kundi la mwisho la wanafunzi linavyojiandaa kuhitimu mwishoni mwa mwaka huu, Programu ya Kilimo Viwanda inaacha alama ya kudumu. Kwa kuwawezesha vijana, kuimarisha ujuzi wa kilimo, na kuwasaidia wakulima wa ndani, programu hii inaonesha wazi jinsi uwekezaji wa kimkakati katika elimu unavyoweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa, kuimarisha usalama wa chakula, na kuendeleza ukuaji wa viwanda kwa njia endelevu

