The House of Social Media
gunners X

Waangalizi wa EAC Waipongeza Uganda kwa Uchaguzi wa Amani

0

Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeipongeza Serikali na wananchi wa Uganda kwa kuendesha Uchaguzi Mkuu wa Januari 2026 kwa amani, huku ukiainisha changamoto kadhaa za kiufundi na kisheria zinazohitaji kufanyiwa kazi katika chaguzi zijazo.

Katika taarifa yao ya awali, waangalizi hao walisema kuwa uchaguzi huo uliendeshwa chini ya mfumo imara wa kikatiba na kisheria, unaozingatia viwango vya kikanda na kimataifa vya misingi ya kidemokrasia.

Ujumbe huo ulihusisha waangalizi 58 wa EAC, wakiongozwa na Balozi Edda Mukabagwiza wa Rwanda, ambao walipelekwa katika maeneo mbalimbali ya Uganda kushuhudia mchakato mzima wa uchaguzi, kuanzia kampeni, upigaji kura, kuhesabu hadi kujumlisha matokeo katika vituo 184 vya kupigia kura.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mazingira ya uchaguzi yalikuwa ya amani kwa ujumla, ingawa vituo vingi vilifunguliwa kwa kuchelewa hadi saa tatu asubuhi kutokana na kuchelewa kwa vifaa vya uchaguzi pamoja na hitilafu za mitambo ya uthibitishaji wa wapiga kura.

Licha ya changamoto hizo, waangalizi walisema kuwa upigaji kura uliendelea kwa utulivu na uwazi, huku maafisa wa uchaguzi na vyombo vya ulinzi na usalama vikionesha weledi katika kutekeleza majukumu yao.

Ujumbe wa EAC pia ulisifu Tume ya Uchaguzi ya Uganda kwa maandalizi ya mapema, ukibainisha kuwa kulikuwa na ongezeko la asilimia 17 ya wapiga kura waliosajiliwa ikilinganishwa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021. Aidha, wanawake walichangia asilimia 53 ya wapiga kura, hali iliyotajwa kuwa ishara chanya ya ushiriki wa kijinsia katika mchakato wa kidemokrasia.

Hata hivyo, waangalizi walionesha wasiwasi kuhusu idadi kubwa ya kura zilizoharibika, pamoja na ukosefu wa takwimu zilizogawanywa kwa jinsia na umri wa wagombea, hali iliyodhoofisha uchambuzi mpana wa ushiriki wa makundi mbalimbali.

Pia walikosoa hatua ya kusitishwa kwa huduma za intaneti siku ya uchaguzi, wakisema ilikwamisha upatikanaji wa taarifa, ufuatiliaji wa uchaguzi na uhuru wa mawasiliano.

Katika mapendekezo yao, ujumbe wa EAC ulitoa wito wa kufanyika kwa marekebisho ya sheria za ufadhili wa kampeni, kuimarishwa kwa elimu ya mpiga kura, kuboreshwa kwa mifumo ya utatuzi wa migogoro ndani ya vyama vya siasa, pamoja na kuimarishwa kwa maandalizi ya kiufundi katika chaguzi zijazo.

Leave A Reply