The House of Social Media
gunners X

Ulaya Yakataa Vitisho vya Ushuru wa Trump Kuhusu Greenland

0
Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen.

Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, amesema kuwa Ulaya haitakuwa chini ya shinikizo la vitisho vya ushuru vilivyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump, kufuatia msimamo wake wa kutaka kununua Greenland.

Kauli hiyo inakuja baada ya Trump kutangaza kuwa atapandisha ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa kutoka nchi nane za Ulaya washirika wa Greenland iwapo zitaendelea kupinga mpango wake wa kuchukua eneo hilo. Frederiksen, kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Ulaya, walitoa taarifa ya pamoja wakionya kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha uhusiano wa Atlantiki na kusababisha mgogoro mkubwa wa kidiplomasia.

Trump amesisitiza kuwa Greenland ni eneo la kimkakati kwa usalama wa Marekani, akieleza kuwa Washington italipata eneo hilo “kwa njia rahisi au ngumu”.

Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema kuwa ongezeko la ushuru wa asilimia 10 litaanza Februari 1, likihusu bidhaa zote zinazoingia Marekani kutoka Denmark, Ufaransa, Uholanzi, Ujerumani, Finland, Norway, Sweden na Uingereza. Ameongeza kuwa ushuru huo unaweza kuongezeka hadi asilimia 25 ifikapo Juni, hadi pale “makubaliano kamili ya kununua Greenland yatakapokamilika”.

Kwa upande wao, viongozi wa nchi hizo nane wamesisitiza ushirikiano wao kamili na Ufalme wa Denmark pamoja na wananchi wa Greenland, wakieleza kuwa usalama wa eneo la Arctic ni maslahi ya pamoja ya NATO na haupaswi kutumika kama chombo cha shinikizo la kiuchumi.

Frederiksen aliandika kupitia ukurasa wake wa Facebook akisema:

“Tunataka kushirikiana, lakini hatutafuti mzozo. Ninafurahi kuona ujumbe thabiti kutoka bara lote: Ulaya haitashinikizwa.”

Trump ameonesha nia ya kununua Greenland kutokana na utajiri wa rasilimali muhimu zilizopo katika eneo hilo, ikiwemo madini na mafuta, pamoja na nafasi yake ya kimkakati kati ya Amerika Kaskazini na Arctic, jambo linaloifanya kuwa muhimu katika usalama wa anga, ufuatiliaji wa silaha na harakati za kijeshi katika ukanda wa Arctic.

Stori na Elvan Stambuli, Global Digital

MZEE BUTIKU KUHUSU MAUAJI ya MZEE KIBAO -”UNATULETEA MAITI AFU UNAKUJA KUHUBIRI DINI – WANGEMPIGA”

Leave A Reply