Mawazo Adaiwa Kumuua Mwenzake na Kupora Pikipiki – Video

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Mawazo Msangawale, Miaka 24, Mkazi wa Mlowo Wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe kwa tuhuma ya mauaji ya kijana wa miaka 18 aitwaye Juveni Baraka Mwambugi aliyekuwa Mkazi wa Isoko Wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya.
Awali, Januari 9, 2026 saa 2 asubuhi katika Kitongoji cha Isoko, Kijiji cha Igundu, Kata ya Sangambi, Tarafa ya Kiwanja, Wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya, Juveni Baraka Mwambugi, miaka 18, mkazi wa Isoko ambaye kwa sasa ni marehemu alipigiwa simu na Mawazo Msangawale akimtaka amfuate porini kwenye mto Mapogoro kwa lengo la kwenda kumuuzia madini aina ya dhahabu.
Toka siku hiyo hakuonekana tena hadi alipokutwa ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye makali kichwani ambapo pia Pikipiki aliyokuwa anatumia yenye namba za usajili MC 599 FJJ aina ya Haojue pamoja na fedha taslimu shilingi 1,500,000/= alizokuwa nazo hazikuonekana eneo la tukio.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia Askari wa kuchunguza matukio ya mauaji, walianza msako mkali na Januari 15, 2026 saa 9 alasiri eneo la Mpemba katika Mji Mdogo wa Tunduma Mkoa wa Songwe walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Mawazo Msangawale, Miaka 24, Mkazi wa Mlowo aliyekuwa akitafutwa kutokana na tuhuma za mauaji haya.
Mtuhumiwa alikutwa akiwa na Pikipiki MC 599 FJJ aina ya Haojue aliyeipora baada ya kutekeleza mauaji haya. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya kujipatia mali na fedha kwa njia isiyo halali. Upelelezi unakamilishwa ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.

