
KANISA la Mlima wa Moto la Mikocheni jijini Dar es Salaam, limezindua kongamano la siku nane la kuombea nchi amani lijulikanalo kama Anza Mwaka na Bwana, ambapo pamoja na maombi, masuala ya ujasiriamali yatapewa kipaumbele.
Akizungumza leo kanisani hapo, Askofu wa kanisa hilo, Rose Mgeta, alisema kongamano hilo linalenga kuliombea taifa amani ili lisirejee kwenye machafuko kama yale ya Oktoba mwaka jana.
Alisema kuwa katika kongamano hilo, vijana watapatiwa mafundisho ya ujasiriamali na biashara ili waweze kutambua fursa zilizopo na kuzitumia kujiondoa kwenye umaskini.
“Mbali na neno la Mungu, vijana watapata elimu ya mbinu mbalimbali za kujipatia kipato, ikiwemo ujasiriamali na namna ya kutumia fursa za kibiashara zilizopo,” alisema Askofu Mgeta.
Aidha, alisema kuwa maadili kwa sasa yameporomoka, hivyo kongamano hilo litatumika pia kuwakumbusha vijana umuhimu wa kuzingatia maadili mema, ikiwemo kuwaheshimu wazazi na watu wanaowazunguka.
“Vijana wanapaswa kuishi maisha ya heshima kwa wazazi na kwa jamii inayowazunguka ili wapate heri duniani. Kuheshimu wazazi ni baraka, hivyo tutawakumbusha umuhimu wa kuwakumbuka na kuwasaidia wazazi wao,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mlimba (CCM), Dk. Hellen-Rose Rwakatare, akitoa shukrani zake baada ya kufanikiwa kupata ubunge, aliwataka waumini kuomba kwa bidii sambamba na kufanya kazi kwa juhudi ili waweze kufanikiwa.
“Maandiko matakatifu yanasema usiposhukuru kwa kidogo hutapewa hata kilicho kikubwa. Nina sababu zote za kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kupata ushindi mkubwa kuanzia kura za maoni hadi Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Alisema kuwa ushindi alioupata haujawahi kutokea katika jimbo hilo baada ya kushinda kwa asilimia 95.9 ya kura.
“Ninamshukuru sana Askofu Rose Mgeta na Askofu Dunstan Maboya ambao waliomba na kuniombea kwa kuniwekea mikono kichwani, wakisema baraka za mama ziko juu yangu. Nawashauri muishi kwa kutenda mema kwa sababu mema hulipa,” alisema.
Aliongeza kuwa mama yake alikuwa mtu wa kutenda mema, jambo lililowasaidia watoto wake kufunguliwa milango kila walikopita.
“Kama una nafasi ya kutenda jema, tenda bila kusubiri shukrani. Hata adui yako mtendee mema. Msikimbie kubadilisha makanisa, ombeni mkiwa hapo hapo, Mungu ni yule yule,” alisema.
Aliwahimiza waumini kuomba kwa vitendo na si kukaa bila kufanya kazi.
“Usiombe ukiwa umekaa bila kufanya kazi. Unaomba kazi lakini unakaa nyumbani, kazi itakujiaje? Unaomba kupandishwa cheo lakini hufanyi kazi kwa bidii, cheo huwezi kupata,” alisema.
Aliwataka pia vijana kujiandaa binafsi wanapoiomba Mungu.
“Msichana unaomba mchumba, jitahidi upendeze. Kijana unaomba mchumba, jitahidi uwe na tabia njema. Mungu anabariki kazi ya mikono, hawezi kubariki uvivu,” alisema.
Alisisitiza kuwa hakuna lisilowezekana chini ya madhabahu, akieleza kuwa wengi waliombewa kanisani hapo wameondokana na umaskini.




