Benki ya Absa Tanzania Tanzania imezindua rasmi ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika 2025 kwa Tanzania katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam Leo.
Hafla hiyo imewakutanisha watunga sera wakuu, wasimamizi wa sekta ya fedha, viongozi wa taasisi za kifedha pamoja na wakurugenzi wa mashirika ya umma na binafsi kujadili hali ya masoko ya fedha barani Afrika na nafasi ya Tanzania katika taswira hiyo.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa Bw. Emmanuel Akaro, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aliyemwakilisha Mheshimiwa Emmanuel Tutuba, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
Uzinduzi wa ripoti hiyo pia ulihudhuriwa na wadau kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Wizara ya Fedha, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), viongozi wa sekta ya umma na binafsi, Bodi na Wakurugenzi na Menejimenti ya Juu ya Absa Bank Tanzania pamoja na wawakilishi wa vyombo vya habari.
Sasa ikiwa katika mwaka wake wa tisa, Ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika, hutumika kama kipimo cha maendeleo ya masoko ya fedha katika nchi 29 za Afrika, zinazowakilisha takribani asilimia 80 ya idadi ya watu na Pato la Taifa (GDP) la bara la Afrika. Ripoti hiyo huandaliwa kwa ushirikiano na Official Monetary and Financial Institutions Forum (OMFIF) na kuungwa mkono na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA).

Tathmini hufanywa kwa kuzingatia nguzo sita kuu zikiwemo kina cha soko, upatikanaji wa fedha za kigeni, uwazi wa soko, maendeleo ya mifuko ya pensheni, mazingira ya uchumi jumla na utekelezwaji wa mifumo ya kisheria.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser, alisisitiza umuhimu wa masoko ya fedha imara na yenye uwazi katika kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi.
“Ripoti ya Afrika ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika ilianzishwa ili kutoa tathmini huru na ya kitaalamu kuhusu mwelekeo wa masoko ya fedha barani Afrika,” alisema Bw. Laiser.
“Kadri uchumi wa Afrika unavyoendelea kukua na kubadilika, masoko ya fedha yaliyo na kina, uwazi na ufanisi ni muhimu katika kukusanya mitaji, kusaidia biashara na kuwezesha maendeleo endelevu.”
Wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya Ripoti ya 2025, wasemaji wakuu kutoka Absa Group walibainisha kuwa, licha ya changamoto za uchumi wa dunia, masoko mengi ya fedha barani Afrika yameonesha maendeleo ya kutia moyo. Mageuzi katika uwazi, mifumo ya udhibiti, utofauti wa bidhaa za kifedha na ubunifu wa kidijitali yalitajwa kuwa nguzo muhimu za kuimarisha ustahimilivu wa masoko.
Akizindua ripoti hiyo, Bw. Emmanuel Akaro aliipongeza ripoti hiyo kama chombo muhimu cha kutathmini sera na kupima maendeleo, huku akirejea nafasi ya Tanzania kama ilivyoainishwa kwenye ripoti hiyo.
“Ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika, inatoa mwanga muhimu kuhusu hatua ambazo Tanzania imepiga katika kuimarisha masoko yake ya fedha,” alisema Bw. Akaro.
“Ripoti inaonesha maeneo ambayo tumefanya vizuri, hususan katika uthabiti wa uchumi jumla na uwazi, lakini pia inaainisha wazi maeneo yanayohitaji maboresho zaidi, ikiwemo kuongeza ushiriki wa wawekezaji wa ndani, kuendeleza mifuko ya pensheni, na kuimarisha mifumo ya kisheria na taasisi.”
Akaro alisisitiza dhamira ya Serikali, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kutekeleza mageuzi yatakayoongeza kina cha masoko, kupanua wigo wa vyombo vya kifedha na kuifanya mifumo ya fedha ya Tanzania kuendana na viwango vya kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Bi. Lulu Ngwanakilala, akimwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Absa Tanzania, Paul Makanza, aliipongeza mijadala yenye tija na ushiriki mkubwa wa wadau.