CCM Bukoba Mjini Yakabidhi Msaada kwa Watoto Yatima Kuelekea Miaka 49 ya Chama
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukoba Mjini imekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali kwa vituo viwili vya kulelea watoto yatima, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 49 ya kuasisiwa kwa chama hicho tawala nchini.
Vituo vilivyonufaika na msaada huo ni Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Hamugembe pamoja na Kituo cha Kashai, ambavyo vinahudumia watoto wenye uhitaji maalum katika Manispaa ya Bukoba.
Msaada uliotolewa unajumuisha mahitaji muhimu ya kila siku, yakiwemo vyakula kama mchele, sukari na unga, pamoja na sabuni kwa ajili ya usafi. Aidha, CCM imekabidhi vifaa vya masomo ikiwemo madaftari, kalamu na penseli, ikiwa ni hatua ya kusaidia watoto hao kuendelea na masomo yao bila vikwazo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Bukoba Mjini, Shaban Mdohe, amesema chama hicho kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya kimepokea changamoto mbalimbali zilizoelezwa na uongozi wa vituo hivyo na kuahidi kuzifanyia kazi.
Miongoni mwa changamoto zilizobainishwa ni upatikanaji wa bima ya afya kwa watoto wanaolelewa katika vituo hivyo, ambapo Mdohe amesema suala hilo litafanyiwa kazi ili kuhakikisha watoto hao wanapata huduma bora za afya kwa wakati.
Ameongeza kuwa maadhimisho ya miaka 49 ya CCM hayatalenga sherehe pekee, bali yatahusisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijamii zenye manufaa kwa jamii.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Chama Cha Mapinduzi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kuchangia ustawi wa makundi yenye uhitaji maalum, sambamba na kuimarisha mshikamano kati ya chama, serikali na wananchi.

