
Kawe, Kinondoni – Februari 7, 2026
Jamii ya Kata ya Kawe, Wilaya ya Kinondoni, imekutana katika mdahalo wa kipekee kujifunza na kubadilishana maarifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kilichojulikana kama Mgahawa wa Maarifa, kilichoandaliwa tarehe 7 Februari 2026.
Mdahalo huu uliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali MyLEGACY kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania kupitia Mradi wa υ, ukilenga kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi kwa makundi yaliyo hatarini zaidi hususan wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu.
Mdahalo huo ulifanyika katika Ofisi za Kikundi cha Wajasiriamali Walemavu Kawe (WAWAKA) na kuwakutanisha wanawake, wazazi, vijana, viongozi wa jamii pamoja na watu wanaoishi na ulemavu.
Kupitia majadiliano ya wazi na shirikishi, washiriki walichambua namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri maisha ya kila siku, yakichochea changamoto za kijamii kama ukosefu wa usalama, ongezeko la ukatili wa kijinsia na kuvuruga upatikanaji wa haki za afya ya uzazi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mwenyekiti wa WAWAKA Bw. Mrisho Bilal alisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji, akisema:
“Kwa muda mrefu watu wenye ulemavu tumekuwa tukiachwa nje ya mijadala ya tabianchi, ilhali sisi ndiyo tunaathirika zaidi wakati wa mafuriko, ukame au majanga mengine. Leo tumepata nafasi ya kusema na kusikilizwa.”
MyLEGACY, kupitia wawakilishi wake, ilieleza kuwa Mgahawa wa Maarifa umebuniwa kama jukwaa salama la sauti za jamii.
“Hatuwezi kujenga ustahimilivu wa tabianchi bila kusikiliza sauti za wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu. Suluhisho lazima yatokane na jamii yenyewe,” alisema Amina Alliy Mtengeti, Mratibu wa Programu kutoka MyLEGACY.

Majadiliano yaligusia kwa kina uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi na masuala ya kijinsia.
Mmoja wa washiriki wanawake alishuhudia kuwa changamoto hizo zinaonekana moja kwa moja katika maisha ya kila siku:
“Tunapokosa maji, sisi wanawake tunapata shida kutafuta maji. Hapo ndipo hatari ya ukatili inaanza, lakini mara nyingi hakuna mtu anayeliona hilo kama tatizo la tabianchi,” alisema.

Aidha majadiliano yalibainisha kwa kina mzigo mkubwa wa kazi za malezi na matunzo unaobebwa na wanawake, hasa wanawake wanaoishi na ulemavu na wale wanaolea watoto wenye ulemavu. Mshiriki mmoja alieleza kwa hisia:
‘Wanawake ndio tunabeba mzigo wa kutunza familia wakati wa ukame au mafuriko.
Ukiongeza ulemavu, au kuwa na mtoto mwenye ulemavu, mzigo unaongezeka maradufu lakini msaada hauongezeki.”
Hatari za ukatili wa kijinsia pia zilijadiliwa kwa uzito, hususan kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi. Mshiriki mmoja alisisitiza hatari wanazokumbana nazo watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi:
“Kwa sababu ya mgao wa maji, watu wenye ualbino wanalazimika kwenda kutafuta maji usiku. Huko njiani wanakutana na hatari kubwa ya ukatili wa kijinsia na mashambulizi, lakini hali hii haizingatiwi kama tatizo la tabianchi.”

Aidha, ilielezwa kuwa katika hali za dharura kama mafuriko, watu wenye ulemavu mara nyingi huachwa nyuma. Kiongozi mmoja wa jamii alisema:
“Wakati wa mafuriko au majanga mengine, watu wenye ulemavu hawapati msaada kwa wakati. Kukosa mifumo ya uokoaji jumuishi kunawaweka katika hatari kubwa zaidi.”
Washiriki walisisitiza kwa pamoja umuhimu wa sera na mikakati ya kitaifa na ya jamii kuingiza masuala ya ukatili wa kijinsia na upatikanaji wa haki za afya ya uzazi katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kama alivyoeleza mmoja wa washiriki:
“Hakuna maana ya mikakati ya tabianchi kama haiwalindi wanawake na wasichana dhidi ya ukatili, wala kuhakikisha huduma za afya ya uzazi zinapatikana hata wakati wa majanga.”

Katika mdahalo huu, jamii iliweka maazimio na ahadi za pamoja, ikiwemo kuimarisha ulinzi wa wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu, kuripoti vitendo vya ukatili wa kijinsia, na kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwa mtazamo wa kijinsia na ujumuishaji.
Mradi wa Kesho Njema, unaotekelezwa na MyLEGACY kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland, unalenga kuunganisha masuala ya tabianchi, usawa wa kijinsia, haki za afya ya uzazi na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, kwa lengo la kujenga jamii salama, jumuishi na yenye ustahimilivu.
Kama ilivyosisitizwa katika kikao hicho, “mabadiliko ya tabianchi si suala la mazingira pekee ni suala la maisha na haki za binadamu,” na hivyo yanahitaji ushiriki wa kila mwanajamii katika kuyaandaa na kuyakabili leo kwa ajili ya kesho njema.
Kwa wasomaji wanaotaka kujifunza zaidi au kufundisha na kuelimisha wengine kuhusu mada hii, MyLEGACY imeandaa vifaa mbalimbali vya elimu na uhamasishaji (IEC Materials).
Unaweza kuzipakua kupitia link iliyopo kwenye tovuti rasmi ya MyLEGACY hapo chini 👇🏾.