
Dar es Salaam, Tanzania – 20/02/2026 Asasi isiyo ya kiserikali ya MyLEGACY imekutana na waandishi wa Habari na wadau wa vyombo vya habari katika Kikao cha Ushirikishwaji wa Vyombo vya Habari kwa lengo la kuimarisha uelewa wa umma kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kuiweka sekta ya habari kama jukwaa muhimu la utetezi.
Akizungumza kwenye Kikao hicho Mkurugenzi wa MyLEGACY, Fortunata Temu amesema Kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Kukuza Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Zinazozingatia Usawa wa Kijinsia kwa Kesho iliyo Bora (Kesho Njema), unaotekelezwa kwa msaada wa Embassy of Ireland in Tanzania.
Jamii nchini Tanzania zinaendelea kukabiliwa na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo mafuriko, ongezeko la joto la muda mrefu na uhaba wa maji.
Athari hizi zinawaathiri zaidi wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu. Mabadiliko ya tabianchi yanaongeza pengo la kijinsia lililopo, yanaongeza hatari za ukatili wa kijinsia , na kuvuruga upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi na haki zake.
Pamoja na hali hii, mifumo ya mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi mara nyingi haijumuishi kikamilifu mwelekeo wa kijinsia katika tathmini ya udhaifu na ustahimilivu wa jamii.
Kupitia Mradi wa Kesho Njema, MyLEGACY imefanya kazi katika kata za Kawe, Kunduchi na Wazo Hill, Wilaya ya Kinondoni, kwa lengo la kuimarisha mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inayozingatia usawa wa kijinsia na kuongeza ustahimilivu wa jamii.
Tathmini ya Mipango ya Utekelezaji wa Tabianchi:
Kuhakikisha inaingiza afua za Haki za Afya ya Uzazi na Kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia
Chini ya mradi huu, MyLEGACY ilifanya Tathmini ya Mipango ya ya kushughulikia mabadiliko ya Tabianchi inavyozingatia Haki za Afya ya Uzazi na kuzuia Ukatili wa Kijinsia katika, Wilaya ya Kinondoni – Dar es Salaam mkazo ukiwekwa kwenye shule za msingi na sekondari, Jamii za watu wenye ulemavu na Viongozi wa kwenye jamii.
Tathmini hii ilichambua mipango ya utekelezaji wa tabianchi, mifumo ya shule ya kukabiliana na majanga, na miundo ya utawala wa jamii kuanzia mwaka 2013/14 hadi 2024/25 ili kubaini kiwango ambacho masuala ya haki za afya uzazi na ukatili wa kijinsia yamejumuishwa.
Matokeo Muhimu yaliyojitokeza:
Mipango ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi katika ngazi ya kata inaweka kipaumbele kwenye miundombinu hasa usafishaji na urekebishaji wa mifereji ya majitaka na usafi na utunzaji wa mazingira.
Masuala ya haki ya afya ya uzazi na Ukatili wa Kijinsia hayajajumuishwa ipasavyo katika mifumo rasmi ya mipango ya tabianchi.
Masuala ya kijinsia hayajaingizwa kwa kushughulikiwa kwa utaratibu.
Ushirikiano kati ya idara za mazingira, afya na jinsia bado ni mdogo.
Takwimu zilizoainishwa kijinsia kuhusu athari za tabianchi hazitoshelezi.
Ushiriki wa wanawake, vijana na makundi yaliyotengwa katika maamuzi ya tabianchi ni mdogo.
Tathmini inapendekeza kuingiza viashiria vya haki za afya ya uzazi na kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia katika mikakati ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi ya ngazi za mitaa, kuimarisha uratibu kati ya idara, kuweka bajeti za tabianchi zinazozingatia jinsia, na kupanua ushiriki wa wanawake na vijana katika kwenye masual ya mabadiliko ya tabianchi.
Uhamasishaji Mashuleni: Kuwawezesha Wanafunzi 775 Kuwa Mabalozi wa Tabianchi
Mradi wa Kesho Njema umefikia wanafunzi 775 wanachama wa vilabu vya WASH wenye umri wa miaka 9–17 kutoka shule 25 kupitia vipindi maalum vya uelimishaji kuhusu tabianchi.

Vilabu hivi ni chachu inayotumika kueneza Elimu na Maarifa katika shule ambazo ni washirika wa MyLEGACY. Kupitia midahalo na shughuli za uhamasishaji mashuleni, tumejifunza masuala muhimu yanayoweza kuimarisha utekelezaji wa programu za kijamii na kimazingira katika mazingira ya elimu.
Kwanza, ushirikishwaji wa wadau mapema ni msingi wa utekelezaji wenye ufanisi na unaoendelea kwa urahisi. Changamoto iliyojitokeza ya baadhi ya walimu wakuu wapya kutokuwa na taarifa za awali kuhusu mawasiliano ya mradi imeonesha umuhimu wa kuwa na utaratibu endelevu wa mawasiliano na mamlaka za elimu pamoja na uongozi wa shule.
Kuimarisha uratibu na Maafisa Elimu wa Wilaya na bodi za shule kunasaidia kujenga umiliki wa taasisi, kuondoa mkanganyiko, na kupunguza ucheleweshaji wa utekelezaji wa shughuli.
Pili, mbinu zinazomweka mtoto katikati ya mchakato wa kujifunza huongeza ushiriki na uhifadhi wa maarifa. Matumizi ya mbinu shirikishi na bunifu kama hadithi, kazi za vikundi, igizo na sanaa yameonesha mafanikio makubwa katika kuvutia umakini wa wanafunzi na kuimarisha uelewa wao.
Wanafunzi waliweza kuhusisha ujumbe wa matumizi sahihi ya nishati na maisha yao ya kila siku, na kuonesha uelewa wao kupitia maonesho na michoro, jambo lililodhihirisha kujifunza kwa kina na kwa vitendo.
Tatu, kuunganisha masuala ya kijinsia na kijamii huongeza umuhimu na uhalisia wa mada husika.
Kuunganisha uhifadhi wa nishati na masuala mapana ya mabadiliko ya tabianchi, ukatili wa kijinsia, na haki za afya ya uzazi na uzazi kuliwasaidia wanafunzi kuelewa athari za kimazingira katika maisha ya binadamu. Mtazamo huu jumuishi uliifanya mada kuwa karibu zaidi na uzoefu wao, na kuchochea hisia za uwajibikaji na huruma miongoni mwa wanafunzi.
Nne, kuwawezesha wanafunzi kuwa mawakala wa mabadiliko kunakuza uendelevu wa afua. Wanafunzi wanapopewa majukumu ya uongozi kama “Mabingwa wa Nishati,” hujenga hisia ya uwajibikaji binafsi na kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa wenzao.
Shauku na ubunifu wao vimeonesha wazi kuwa vijana wana uwezo mkubwa wa kuhamasisha mabadiliko ya tabia si tu shuleni bali pia katika jamii wanazotoka, hivyo kuhakikisha matokeo ya muda mrefu na endelevu.
Mgahawa wa Maarifa : Kuimarisha Majadiliano ya Kijamii
MyLEGACY inalo Jukwaa lake na kueneza Maarifa, Elimu na taarifa mbalimbali zikiwemo matokeo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa.
Jukwaa hili linaitwa Mgahawa wa Maarifa.
Tumeshaitisha Migahawa ya Maarifa kadhaa katika Jamii iliyowakutanisha washiriki 249, wakiwemo viongozi wa mitaa, wanawake, vijana, walimu, watu wenye ulemavu na wanajamii kwa ujumla.

Kupitia midahalo hii, tumeweza kujifunza na kuthibitisha mambo kadhaa muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika juhudi za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Kwanza, sauti za jamii ni kichocheo muhimu cha hatua za maendeleo.
Vikao hivi vimedhihirisha kuwa jamii za maeneo husika zina uelewa wa kina kuhusu changamoto zao za kimazingira. Zinapopewa nafasi salama, jumuishi na iliyoandaliwa kwa utaratibu mzuri, wanajamii huweza kubainisha si tu chanzo cha matatizo bali pia kupendekeza suluhisho halisi na yanayotekelezeka, yakitokana na uzoefu wao wa moja kwa moja.
Ushiriki wao si jambo la hiari, bali ni sharti la mafanikio ya afua endelevu na zenye tija.
Pili, mjadala kuhusu mabadiliko ya tabianchi unapaswa kuzingatia mwingiliano wa masuala mbalimbali ya kijamii.
Midahalo imeonesha wazi kuwa tabianchi si suala linalojitegemea pekee, bali lina uhusiano wa karibu na masuala ya kijinsia, ulemavu, elimu na afya. Wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu hukabiliwa na athari za kipekee na mara nyingi zilizounganishwa, zinazowaweka katika hatari kubwa zaidi.
Hivyo, mipango na programu zijazo zinapaswa kubuniwa kwa kuzingatia mtazamo jumuishi unaotambua mwingiliano huo, ili kuhakikisha hakuna anayesahaulika.
Tatu, uelewa pekee hautoshi bila kuwepo kwa mifumo thabiti ya utekelezaji. Ingawa uelewa kuhusu masuala ya mazingira unaongezeka katika jamii, bado kuna pengo kati ya maarifa na hatua za vitendo.
Jamii nyingi hazina mifumo na rasilimali zinazowawezesha kubadili uelewa huo kuwa utekelezaji madhubuti. Hii inajumuisha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa taka, utekelezaji wa kanuni ndogo za mazingira, upangaji wa bajeti jumuishi, pamoja na kuimarisha elimu ya tabianchi shuleni.
Kuna umuhimu wa kuimarisha miundo na sera za taasisi zitakazounganisha utayari wa jamii na uwezo wa utekelezaji kwa ufanisi.
Utekelezaji wa Vitendo kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi
MyLEGACY iliviwezesha vilabu vya Usafi (WASH) na Mazingira mashuleni kupandaji miti, mashuleni na katika jamii za jirani.

Lengo kuu la mpango huu lilikuwa kupunguza ukataji miti na kuimarisha uhifadhi wa mazingira kwa njia endelevu.
Matokeo makuu yaliyotokana na utekelezaji huu ni:
Kuimarisha Mazingira ya Shule Yenye Usawa na Ustawi Bora wa Wanafunzi: Miti 2,000 ya kivuli na matunda ilipandwa katika shule 24. Miti hii inatazamiwa kuboresha mazingira na kupunguza joto na vumbi, na kuwapa wanafunzi vivuli wakati wakihitaji kupumzika au kujifunza na hata kucheza.
Uelewa wa Tabianchi Unaolenga Usawa wa Kijinsia na Kupunguza Hatari za Ukatili wa Kijinsia:
Wanafunzi, hususan wasichana, walipata Elimu na kuongeza uelewa wa jinsi mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri ustawi wa kijamii na kuongeza hatari za ukatili wa kijinsia Ushiriki wa usawa katika shughuli za upandaji miti na utunzaji uliimarisha usalama, kujiamini, na uongozi wa wasichana katika hatua za kukabiliana na tabianchi.
Ujuzi Kivitendo jinsi ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi:
Wanafunzi walipata ujuzi wa vitendo katika upandaji wa miti, kumwagilia, na utunzaji baada ya upandaji, ikiwa ni pamoja na mbinu za gharama nafuu za umwagiliaji kama mfumo wa drip irrigation kwa kutumia chupa za plastiki zinazotumika na kuachwa ovyo na kuchafua mazingira.
Ujuzi huu uliwawezesha kutafsiri maarifa ya tabianchi kuwa vitendo shuleni na nyumbani.
Kuimarisha Uongozi wa Wanafunzi Kupitia Vilabu vya Shule: Wanafunzi wanachama wa Vilabu vya Usafi (WASH) na Mazingira viliongoza zoezi la kuhamasisha wanafunzi kutunza miti, na kufuatiliaji, jambo lililochochea umiliki wa shughuli, uwajibikaji, na uendelevu wa shughuli hizi hata baada ya kipindi cha utekelezaji wa mradi kuisha.
Kuimarisha Ushirikiano Kati ya Shule na Jamii na Utekelezaji Endelevu wa Hatua za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi:
Ushirikiano kati ya wanafunzi, walimu, uongozi wa shule na wanajamii uliimarisha uwajibikaji wa pamoja katika uhifadhi wa mazingira na kuanzisha mifumo ya ufuatiliaji ili kuhakikisha ustawi wa miti na kutoa mwongozo kwa shughuli za tabianchi zinazofuata.
Matokeo haya yanaonesha wazi kuwa mchakato huu wa kushirikisha shule na jamii unaweza kuendeleza uelewa, ustawi wa kijamii, uongozi wa vijana, na hatua endelevu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kuhusu MyLEGACY
MyLEGACY ni shirika lisilo la kiserikali lililojikita katika kutokomeza umaskini uliokithiri katika jamii zilizotengwa kwa kuongeza upatikanaji wa makazi bora, kuwawezesha kiuchumi wanawake na vijana, kukuza uongozi jumuishi wa jamii, na kutetea haki za wanawake na watoto.