
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Machi 3, 2026 ameongoza hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, eneo la Kigamboni Mnadani. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wageni mashuhuri.
Mradi huu ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya nishati na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta kwa uhakika nchini. Matanki haya yatasaidia kupunguza muda meli zinavyosubiri kuingia bandari kutoka wastani wa siku 22 hadi siku 7, pamoja na kupunguza muda wa kushusha shehena ya mafuta kutoka siku 7 hadi siku 1.

Aidha, mradi huu unatarajiwa kuongeza mapato ya Taifa kupitia tozo na huduma za bandari, sambamba na kutoa ajira kwa Watanzania katika hatua za ujenzi na uendeshaji. Ujenzi wa matanki haya pia unalenga kupunguza changamoto za uhaba wa mafuta na kuongeza ufanisi wa usambazaji wake katika sekta ya nishati.
Rais Samia amesisitiza kuwa mradi huu ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa na unaonyesha dhamira ya Serikali katika kuhakikisha miundombinu ya kimkakati inakidhi mahitaji ya wananchi.

