
Dar es Salaam, Machi 9, 2026 – Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania imeandaa hafla maalumu ya Iftari ya mwezi mtukufu wa Ramadan jijini Dar es Salaam, ikiwakutanisha viongozi wa serikali, wateja, wadau na wanahabari katika mazingira ya mshikamano, tafakari na shukrani.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Khamis Mussa Omar, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, na wageni wengine waalikwa kutoka sekta mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kamoto aliwashukuru wateja, wadau na washirika wa kampuni hiyo kwa kuendelea kuiamini Airtel, akisema mchango wao umekuwa msingi muhimu katika ukuaji wa kampuni na kuimarisha huduma zake kote nchini.
“Ramadan ni kipindi cha tafakari, kujitolea na kuimarisha mshikamano. Tunafurahia kushiriki wakati huu maalumu na wateja na washirika wetu ambao wanaendelea kutuunga mkono katika safari yetu ya kuunganisha Tanzania,” alisema Kamoto.
Alisema Airtel Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupanua huduma zake, ikiwemo kufikisha wateja zaidi ya milioni 23 nchini. Pia alieleza kuwa kampuni imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya mawasiliano kwa kuongeza vituo vya mitandao ya 4G na 5G ili kuboresha upatikanaji wa huduma za intaneti.

Kwa mujibu wa Kamoto, mtandao wa 4G wa Airtel sasa unafunika zaidi ya asilimia 90 ya maeneo ya Tanzania, jambo linalochangia upatikanaji wa huduma za intaneti kwa kasi na kusaidia juhudi za nchi kuelekea uchumi wa kidijitali.
Katika kuboresha huduma kwa wateja, kampuni hiyo pia imepanua mtandao wa maduka yake kwa kufungua maduka mapya 31 kote nchini ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Kamoto aliongeza kuwa huduma ya Airtel Money imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kukuza ujumuishaji wa kifedha, kwa kuwawezesha mamilioni ya Watanzania kupata huduma za kifedha kupitia simu zao za mkononi.
“Kupitia Airtel Money, tunaleta huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi na kusaidia kupunguza pengo kati ya jamii za mijini na vijijini,” alisisitiza.

Aidha, alisema Airtel Tanzania imeendelea kusaidia biashara ndogo na za kati (SMEs) kwa kutoa suluhisho za kidijitali na huduma za mawasiliano zinazowezesha biashara hizo kukua na kushindana katika soko la kisasa.
Kwa upande wake, Waziri Khamis Mussa Omar aliipongeza Airtel Tanzania kwa uwekezaji wake katika miundombinu ya mawasiliano na mchango wake katika kukuza uchumi wa nchi.
Alisema sekta ya mawasiliano ina mchango mkubwa katika kuunda ajira, kusaidia biashara na kuongeza mapato ya serikali.
Waziri huyo pia alisisitiza kuwa serikali inaendelea kushirikiana kwa karibu na kampuni hiyo, akibainisha kuwa Serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 49 ya hisa katika Airtel Tanzania.
Aidha alimpongeza Airtel kwa kufanikisha upanuzi wa mtandao wa 4G kufikia zaidi ya asilimia 90 nchini pamoja na kuanzisha teknolojia ya 5G, akisema hatua hiyo inawawezesha zaidi ya wateja milioni 23 kupata huduma bora za mawasiliano na fursa za kiuchumi.
Pia aliipongeza huduma ya Airtel Money kwa kusaidia juhudi za ujumuishaji wa kifedha, akisema jukwaa hilo limefikia watumiaji zaidi ya milioni 14 nchini.
Waziri Omar alithibitisha dhamira ya serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali na kuharakisha mabadiliko ya kidijitali nchini chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hafla hiyo ya Iftari imeonyesha dhamira ya Airtel Tanzania ya kuimarisha ushirikiano na wadau wake huku ikiendelea kuchangia maendeleo ya uchumi jumuishi na mageuzi ya kidijitali nchini.
