×

Kihongosi: Chama Cha Mapinduzi Ndiyo Baba wa Demokrasia – Video

Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi

Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amesema CCM ndiyo baba wa demokrasia nchini kwani ndiyo chanzo cha kuzaliwa kwa vyama vingine vya siasa na utawala wa vyama vingi.

Kihongosi amesema hayo Machi 8, 2026 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Lagangabilili wilayani Itilima mkoani Simiyu.

Akizungumza hayo Kihongosi amesema kabla ya kuzaliwa kwa vyama vingine vya siasa, akisema ilianza Tanganyika African National Union (TANU) 1954 na baada ya muungano Februari 5,1977 ikaundwa CCM ambacho ndicho kilizaa siasa ya vyama vingi 1992 lakini bado kimeendeleo kuwa kinara na chama namba moja nchini.

Amesema na muasisi wa vyama vingi ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye hata baada ya kura za ndio kwa siasa za vyama vingi kuwa chache bado alitaka kuwe na mfumo huo, hali inayothibitisha ukomavu wa demokrasia wa chama hicho.

Amesisitiza vyama vingine vidogo vimekuwa vikiendeshwa kama saccos hali inayotofautisha CCM na vyama vingine kwani ni chama kikubwa na chenye uzoefu wa miaka mingi.

 

Amesema uongozi wa nchi unahitaji watu wenye uzoefu, maarifa na uwezo wa kufanya maamuzi makubwa na kusimamia masuala ya maendeleo kwa manufaa ya taifa. Alifananisha uongozi wa nchi na dereva wa gari kubwa, akieleza kuwa kama ilivyo kwa madereva wa malori au mabasi makubwa wanaohitaji uzoefu mkubwa, ndivyo ilivyo pia kwa uongozi wa taifa.

“Hawa waliokwisha kuendesha magari makubwa kwa miaka mingi wana uzoefu. Ukimpa mtu ambaye hajazoea kuendesha gari kubwa anaweza kushindwa kulimudu,” amesema Kihongosi.

Amesema wananchi ni mashahidi kuwa CCM imelitoa taifa hili mbali na ndiyo maana wanapata sababu ya kushinda chaguzi nyingi kwani wamekuwa wakitekeleza yake ambayo wamekuwa wakiyaahidi kupitia ilani ya uchaguzi.

Leave a Comment