×

Prof. Kitila Awasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2026/27

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Kitila Alexander Mkumbo amewasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/2027, akieleza kuwa mpango huo utalenga kuimarisha uchumi jumuishi, kuongeza ajira na kuharakisha maendeleo ya taifa.

Akiwasilisha mpango huo katika mkutano wa wabunge wote, Profesa Mkumbo alisema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31) na pia ni hatua ya kuanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mpango wa mwaka 2026/27 utaongozwa na dhima ya “Mageuzi kwa ajili ya Ukuaji Jumuishi wa Uchumi na Uzalishaji Ajira.”

Uchumi wa Tanzania waendelea kuimarika

Profesa Mkumbo alisema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha, ambapo katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2025, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.0 ikilinganishwa na asilimia 5.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2024.

Alisema ukuaji huo umechangiwa na uwekezaji wa serikali katika miradi mikubwa ya miundombinu ya nishati, maji na usafirishaji, pamoja na kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji katika sekta za kilimo, viwanda na madini.

Aidha, mfumuko wa bei nchini uliendelea kuwa katika kiwango kinachodhibitika cha wastani wa asilimia 3.3 mwaka 2025, ndani ya lengo la taifa la asilimia 3 hadi 5.

Mafanikio ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo

Serikali imesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali umechangia kuimarika kwa huduma na shughuli za kiuchumi.

Baadhi ya mafanikio yaliyotajwa ni pamoja na:

  • Kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme hadi megawati 4,504.54 mwaka 2025/26

  • Kuongezeka kwa watalii kufikia zaidi ya milioni 5.9

  • Kuongezeka kwa eneo la umwagiliaji hadi hekta 983,466

  • Kuimarika kwa usafirishaji wa mizigo kupitia reli

  • Kuongezeka kwa upatikanaji wa maji safi vijijini.

Vipaumbele vya Mpango wa 2026/27

Serikali imeainisha maeneo makuu matano ya kipaumbele katika mpango huo ambayo ni:

  1. Kuimarisha utawala bora, demokrasia, amani na utulivu

  2. Kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani

  3. Kuimarisha uwezo wa watu na maendeleo ya jamii

  4. Kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

  5. Kuimarisha vichocheo vya mageuzi ikiwemo nishati, miundombinu na teknolojia ya kidijitali.

Gharama za mpango

Serikali imekadiria kuwa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27 utagharimu shilingi trilioni 86.3.

Kati ya fedha hizo:

  • Sekta binafsi itachangia takribani shilingi trilioni 60.1 (asilimia 69.6)

  • Sekta ya umma itachangia shilingi trilioni 26.2 (asilimia 30.4).

Profesa Mkumbo alisema ushiriki wa sekta binafsi utakuwa muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Malengo ya kiuchumi

Serikali inalenga kufikia malengo kadhaa ifikapo mwaka 2026/27, ikiwemo:

  • Ukuaji wa uchumi kufikia asilimia 6.3

  • Kuzalisha ajira milioni 1.7

  • Kuongeza uzalishaji wa umeme hadi megawati 4,654.5

  • Kuongeza eneo la umwagiliaji hadi hekta milioni 1.2.

Profesa Mkumbo alisema serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na inaleta matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi.

Bofya hapa kusoma MAELEZO YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI, MHESHIMIWA PROF. KITILA ALEXANDER MKUMBO (MB), AKIWASILISHA KWENYE MKUTANO WA WABUNGE WOTE MAPENDEKEZO YA SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2026/27

Leave a Comment