×

Rostam Aziz Anunua Hisa za Nation Media Group kutoka AKFED

Mfanyabiashara wa Tanzania Rostam Aziz

Aga Khan Fund for Economic Development imetangaza kufikia makubaliano ya kuuza hisa zake zote katika Nation Media Group kwa mfanyabiashara wa Tanzania Rostam Aziz kupitia kampuni yake ya Taarifa Limited.

Katika taarifa rasmi, AKFED imesema imeingia makubaliano ya kuuza asilimia 100 ya umiliki wake wa hisa asilimia 54.08 katika kampuni ya NPRT Holdings Africa Limited, ambayo ndiyo kampuni inayoshikilia hisa za AKFED ndani ya Nation Media Group (NMG).

Kupitia ununuzi huo, Rostam Aziz sasa anakuwa mbia mkubwa (majority shareholder) wa kampuni hiyo ya vyombo vya habari, akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Aga Khan Fund for Economic Development.

Kupitia NPRT, AKFED ilikuwa inamiliki jumla ya hisa za kawaida 92,618,177, ambazo ndizo zilizompa Aziz nafasi ya kuwa mbia mkuu wa kampuni hiyo ya habari.

Ingawa thamani kamili ya fedha za mkataba huo haijawekwa wazi, hatua hiyo imemthibitisha Rostam Aziz kuwa mmiliki mkubwa wa Nation Media Group.

Uuzaji huo pia unahitimisha uhusiano wa miaka 66 kati ya NMG na AKFED, ushirikiano ambao ulianza mwaka 1959, ukionekana kama ndoa ya muda mrefu katika historia ya kampuni hiyo ya vyombo vya habari Afrika Mashariki.

Jengo la makao makuu ya Nation Media Group linaitwa Nation Centre, na linapatikana kwenye mtaa wa Kimathi katikati ya Nairobi CBD nchini Kenya.

Nation Media Group ni kampuni mama ya Mwananchi Communications Limited, inayochapisha magazeti maarufu nchini Tanzania ikiwemo The Citizen, Mwananchi, na Mwanaspoti.

Nje ya Tanzania, NMG pia inamiliki Monitor Publications Limited nchini Uganda, ambayo huchapisha gazeti la Daily Monitor.

Nchini Kenya, Nation Media Group huchapisha magazeti kadhaa yanayoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, yakiwemo Daily Nation, Business Daily, The EastAfrican, pamoja na gazeti la Kiswahili Taifa Leo.

Mbali na vyombo vya habari vya magazeti na majukwaa ya kidijitali, kampuni hiyo pia inaendesha vituo vya utangazaji kama NTV Kenya, NTV Uganda, KFM, na Nation FM.

Kupitia uwepo wake katika magazeti, majukwaa ya kidijitali, televisheni na redio katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki, Nation Media Group imekua na kuwa moja ya kampuni kubwa zaidi za vyombo vya habari binafsi barani Afrika.

VYAMA VYA SIASA VIKO WAPI?-KWANINI KATIBA MPYA?-KUNA UMUHIMU MABADILIKO BARAZA MAWAZIRI?

Leave a Comment