
Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha Usalama barabarani Mkoani Arusha limetoa mafunzo maalumu ya mfumo mpya wa TEHAMA juu ya usimamizi na usajili wa shule za udereva kwa wakuu wa vyuo na wakufunzi wa vyuo hivyo lengo likiwa ni kupata madereva wenye bora na kupunguza au kuondoa kabisa ajali barabarani.
Akizungumza mara baada ya kufungua Mafunzo hayo leo, Mkuu wa Polisi Jamii mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Salvas Makweli kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoani humo amesema mifumo ya ufundishwaji katika vyuo vya udereva inapaswa kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

ACP Makweli amebainisha kuwa wasimamizi wa vyuo vya udereva wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuepuka udanganyifu wakati wakitoa mafunzo kwani wasipofanya hivyo watakuwa wanakiuka sheria.
Sambamba na hilo, amewasihi wakufunzi hao pindi wanapokuwa wanatoa mafunzo vyuoni, kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika suala la usalama barabarani huku akitolea mfano madhara ya mwendokasi, ulevi uzembe pamoja na sheria za usalama barabarani.
Pia, amewataka kuhakikisha wanakwenda kusimamia nidhamu ili kuwapata madereva wazuri wenye maadili na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya udereva na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Zauda Mohamed amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni katika kuhakikisha wanazalisha madereva wenye ubora ambao watasaidia kupunguza ajali za barabarani.
ACP Zauda amebainisha kuwa, kupitia mfumo huo mpya, wataweza kusimamia ipasavyo vyuo vya udereva kuanzia kipindi ambacho mwanafunzi anaandikishwa chuoni, mwenendo mzima wa wakufunzi na chuo kwa ujumla hali ambayo itasaidia kuondoa madereva wasiokuwa na sifa hasa wenye vyeti feki.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha Dkt. Florence Mamboya amesema mfumo huo utaenda kuleta tija kwenye usalama wa vyombo barabarani kwani utasaidia kuweka kumbukumbu sahihi za madereva kuanzia shule aliyosoma, mkufunzi aliyemfundisha na mwaka ambao amemaliza.