×

Stanbic Yatajwa Benki Bora ya Kimataifa kwa Wateja Maalum

Dar es Salaam, 23 Machi 2026 – Benki ya Stanbic imepata tuzo tatu za kimataifa kutoka jarida la Euromoney ambazo ni Benki Bora ya Kimataifa kwa Wateja Maalum, Benki Bora kwa Kizazi Kijacho, na Benki Bora kwa Huduma kwa Wateja, zikionesha mafanikio yake katika kusaidia wateja kujenga, kukuza na kulinda mali zao kwa mtazamo wa muda mrefu.

Tuzo hizo zilitolewa katika hafla ya Euromoney Private Banking Awards 2026 iliyofanyika London, baada ya tathmini iliyofanywa na jopo huru la wataalamu wa sekta ya fedha. Hii ni mara ya pili mfululizo Stanbic kutambuliwa kama Benki Bora ya Kimataifa kwa Wateja Maalum.

Utambuzi huo unakuja wakati uchumi wa Tanzania ukiendelea kukua na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za usimamizi wa mali, uwekezaji na mipango ya urithi, hasa kwa wajasiriamali na biashara za kifamilia.

Mtendaji Mkuu wa Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira, alisema tuzo hizo zinaonesha umuhimu wa kupanga, kulinda na kurithisha mali kwa ufanisi kwa vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Wateja Maalum, Omari Mtiga, alisema benki inaendelea kuimarisha huduma zinazolenga mahusiano ya muda mrefu na ushauri wa kifedha unaoendana na mahitaji ya kila mteja.

Aidha, Stanbic pia ilitajwa kuwa Benki Bora nchini Tanzania kwa mwaka 2025 na jarida la The Banker, jambo linaloonesha uthabiti wa benki hiyo katika huduma za kifedha.

Leave a Comment