
WADUKUZI wanaodaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na Iran wamezua taharuki kubwa kimataifa baada ya kudai kuidukua akaunti binafsi ya barua pepe ya Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), Kash Patel.
Hatua hiyo, inachukuliwa kama pigo kubwa kwa mifumo ya usalama wa taarifa ya Marekani na ishara ya kuongezeka kwa vita vya kimtandao vinavyoambatana na migogoro ya kisiasa duniani.
Kundi hilo linalojitambulisha kama Handala Hack Team lilitoa taarifa kupitia jukwaa lao la mtandaoni likisema wazi kuwa limefanikiwa kuidukua akaunti hiyo.

Kama uthibitisho wa madai yao, walichapisha mtandaoni picha binafsi zinazodaiwa kuwa za Patel pamoja na nyaraka na mawasiliano mbalimbali, wakionesha kile kinachoonekana kuwa ni mchanganyiko wa taarifa za kikazi na maisha binafsi.
Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Department of Justice, ni kweli uvamizi huo umetokea na baadhi ya nyaraka zilizovuja zinaonekana kuwa halisi.
Hata hivyo, FBI haijatoa tamko rasmi, hali inayoongeza sintofahamu kuhusu ukubwa wa udukuzi huo, kiwango cha taarifa zilizovuja, na kama kuna taarifa nyeti za kiusalama zilizofikiwa na wadukuzi hao.
Kundi la Handala linajitambulisha kama wadukuzi wanaounga mkono Palestina, lakini wachambuzi wa usalama wa kimtandao katika nchi za Magharibi wanaamini kuwa ni moja ya makundi ya kivuli yanayotumiwa na vitengo vya kijasusi vya Iran kutekeleza mashambulizi ya mtandao bila kuhusisha moja kwa moja serikali.