
Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Harmonize, ameibua mjadala mkubwa mitandaoni baada ya kuonekana kujibu kauli iliyotolewa na Msanii nyota wa Bongo Fleva na Mkurugenzi Mtendaji wa WCB Wasafi, Diamond Platnumz, katika mahojiano yake kupitia Wasafi FM, licha ya Diamond kutomtaja moja kwa moja jina lake.
Kupitia Insta Stori yake, Harmonize ameandika ujumbe mrefu wenye ujumbe unaogusa masuala ya kijamii na vipaumbele vya taifa, ambapo amekumbusha kauli ya zamani ya Diamond aliowahi kuwahimiza Watanzania wafanye kazi badala ya kulalamika. Harmonize amesema kuwa sasa inaonekana ni muda wa msanii huyo mwenyewe kuonyesha mfano wa kile alichokuwa anakihimiza.
Katika ujumbe wake, Harmonize amesisitiza kuwa Watanzania wanahitaji zaidi maendeleo muhimu kama elimu, afya, miundombinu ya barabara, pamoja na kuboresha kilimo kupitia upatikanaji wa mbolea kwa wakulima. Aidha, ameongeza kuwa nchi inahitaji uwekezaji zaidi katika huduma za kijamii na siyo mambo yanayoonekana kama burudani au maslahi binafsi ya watu wachache.

Kauli hiyo imeonekana na wengi kama jibu la moja kwa moja kwa mjadala unaoendelea, huku ikizidi kuongeza mvutano wa muda mrefu uliopo kati ya Harmonize na Diamond Platnumz, ambao ulianza tangu Harmonize alipoondoka katika lebo ya Wasafi na kuanza safari yake ya muziki binafsi.
Hadi sasa, Diamond Platnumz hajatoa kauli ya kujibu moja kwa moja ujumbe huo wa Harmonize, lakini mashabiki na wadau wa muziki wanaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mjadala huu unaoendelea kuchukua sura mpya kila siku.