
Rapper maarufu Cardi B ameendelea kuibuka mshindi kisheria baada ya mahakama ya Marekani kutupilia mbali kesi ya madai ya hakimiliki yenye thamani ya dola milioni 50 iliyowasilishwa dhidi yake.
Kwa mujibu wa taarifa, Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Marekani, Fernando Rodriguez, aliamua kufuta kesi hiyo iliyofunguliwa na Joshua Fraustro na Miguel Aguilar dhidi ya Cardi B, wakidai wimbo wake Enough (Miami) ulikiuka hakimiliki na kunakili wimbo wao Greasy Frybread.
Walalamikaji hao walidai kuwa Cardi B alitumia kazi yao bila idhini, hatua ambayo, kwa mujibu wao, ilisababisha madhara kwa sifa zao katika tasnia ya muziki na hata kudaiwa kuepukwa (blacklisting) na baadhi ya wadau wa sekta hiyo.
Hata hivyo, upande wa Cardi B kupitia mawakili wake uliwasilisha hoja kadhaa mahakamani, ukibainisha kuwa wimbo wa “Greasy Frybread” haukuwa umesajiliwa rasmi kwa hakimiliki wakati kesi hiyo inafunguliwa. Usajili huo ulifanyika baadaye, tarehe 31 Oktoba 2025, zaidi ya mwaka mmoja baada ya kesi kuwasilishwa.
Wakili wa Cardi B, Lisa F. Moore, alieleza kufurahishwa na uamuzi wa mahakama, akisisitiza kuwa mahakama ilichunguza kwa makini hoja zote kabla ya kutoa uamuzi huo.
Kesi hii inakuja miezi michache baada ya Cardi B pia kushinda kesi nyingine ya madai ya shambulio na uhalifu wa kimwili iliyofunguliwa na aliyekuwa mlinzi wake, Emani Ellis, ambapo juria ya Los Angeles iliamua kuwa rapper huyo hakuhusika na madai yaliyotolewa dhidi yake.
Ushindi huu mpya unaongeza kwenye historia ya Cardi B ya kushinda kesi mbalimbali mahakamani, huku akiendelea kulinda jina lake na kazi zake katika tasnia ya burudani.