×

Enzo Fernandez Aingia Kwenye Mzozo na Chelsea, Afungiwa Mechi Mbili

Enzo Fernandez

Klabu ya Chelsea FC imemuweka kando kiungo wake nyota Enzo Fernandez kwa mechi mbili kufuatia kauli zake za hadharani kuhusu mustakabali wake ndani ya klabu hiyo.

Uamuzi huo umetangazwa na Kocha Mkuu Liam Rosenior, ambaye amesema Enzo hatakuwepo kwenye mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Port Vale leo pamoja na pambano na mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Manchester City.

Hatua hiyo imekuja baada ya kiungo huyo wa Argentina kusema kuwa ataangalia chaguo baada ya Kombe la Dunia, huku akionyesha wazi kuvutiwa kuishi nchini Spain. Kauli hiyo imeibua mjadala mkubwa ndani na nje ya klabu, hasa ikizingatiwa kuwa Enzo ni mmoja wa viongozi wa timu hiyo kwa sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Rosenior alisema amefanya mazungumzo ya moja kwa moja na mchezaji huyo kabla ya kuchukua uamuzi huo.

“Nilizungumza na Enzo, na kama klabu tumefikia maamuzi kwamba hatakuwa sehemu ya kikosi kwa mechi zijazo. Kauli yake haikuwa sahihi kulingana na maadili na mwelekeo tunaotaka kujenga,” alisema Rosenior.

Enzo, mwenye umri wa miaka 25 na aliyesajiliwa kwa ada kubwa katika historia ya klabu hiyo, amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia klabu kubwa barani Ulaya, ikiwemo Real Madrid, ingawa amekanusha kuwepo kwa mazungumzo rasmi.

Ndani ya Chelsea FC, taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya wachezaji hawakufurahishwa na kauli zake, hasa baada ya pia kuonekana kuwakosoa wenzake uwanjani katika baadhi ya mechi za hivi karibuni.

Kwa sasa, Chelsea inapitia kipindi kigumu baada ya kupoteza mechi kadhaa mfululizo na kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, hali inayoongeza presha kwa kikosi na benchi la ufundi.

Leave a Comment