×

Lalji Foundation Yaendesha Kambi Ya Matibabu Ya Macho Bure Kigoma

Taasisi ya Lalji Foundation, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Kigoma Hilltop Hotel, Ahlulybayt Academic Center, Vision 4 All Eye Centre pamoja na Supa Foam, imeendesha kambi maalum ya siku nne ya matibabu ya macho bure kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma.

Kambi hiyo ilifanyika kuanzia tarehe 03 hadi 06 Aprili 2026 katika viwanja vya Shule za Ahlulbayt Islamic Center, Manispaa ya Kigoma Ujiji. Kupitia kambi hiyo, huduma mbalimbali muhimu zilitolewa, zikiwemo uchunguzi wa macho, ushauri wa kitaalamu, utoaji wa miwani, huduma za dawa, pamoja na upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo.


Akizungumza baada ya kukamilika kwa kambi hiyo, mlezi wa Taasisi ya Lalji Foundation, Mohsen Lalji, amesema zaidi ya wananchi 6,000 walijitokeza kupata huduma. Kati yao, watu 5,079 walifanyiwa uchunguzi wa macho, 2,218 walipatiwa miwani, 518 walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho, na watu 3,215 walipatiwa dawa za macho. Huduma zote zilitolewa bure bila malipo.

Amesema lengo la kambi hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, endelevu, kwa wakati na kwa ukaribu zaidi.

Wakizungumza baada ya kupatiwa huduma, wananchi wengi walieleza kuwa walikuwa hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu ya macho, ikiwemo upasuaji na ununuzi wa miwani, hali iliyowafanya kuendelea kuishi na matatizo ya macho kwa muda mrefu.

Wananchi hao pia waliomba juhudi kama hizi ziendelee kudumishwa ili kuwasaidia watu wengi zaidi, hasa wale wa kipato cha chini ambao bado wanakabiliwa na changamoto ya kumudu gharama za huduma za afya.

Kambi hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za wadau wa maendeleo katika kuhakikisha jamii inapata huduma bora za matibabu ya macho hususan katika maeneo yenye uhitaji mkubwa kama Kigoma.

Leave a Comment