
Wasiwasi umeongezeka katika masoko ya nishati duniani baada ya meli kadhaa za mafuta kuanza kubadili njia na kuepuka kupita katika Mlango wa Hormuz, kufuatia tangazo la Marekani kuanza operesheni ya kuzuia usafiri wa majini unaohusiana na Iran.
Hatua hiyo imechochewa na kushindikana kwa mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Iran mwishoni mwa wiki, hali iliyotikisa matumaini ya kurejea kwa utulivu baada ya kusitishwa kwa mapigano kwa muda wa wiki mbili.
Marekani imethibitisha kuwa itaanza operesheni ya kuzuia meli zinazohusiana na Iran katika Strait of Hormuz kuanzia saa 5:00 usiku (23:00 EAT) leo Jumatatu.

Kwa mujibu wa United States Central Command, zuio hilo litaanza saa 10:00 asubuhi kwa saa za Marekani (14:00 GMT), sawa na saa 5:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Operesheni hiyo inalenga meli zote zinazoingia na kutoka bandari za Iran, lakini Marekani imesisitiza kuwa haitazuia meli zinazopita tu katika njia hiyo kuelekea bandari zisizo za Iran.
Hata hivyo, Marekani imeeleza kuwa haitazuia meli zinazopita tu katika njia hiyo kuelekea bandari zisizo za Iran, ikijaribu kupunguza hofu ya kuvurugika kwa biashara ya kimataifa.

Taarifa za usafirishaji zinaonyesha kuwa baadhi ya meli kubwa zimeanza kuchukua tahadhari mapema. Meli moja kubwa ya mafuta iliyokuwa inaelekea kupakia mafuta kutoka Iraq imelazimika kugeuza mwelekeo na kusimama karibu na Ghuba ya Oman, ikisubiri hali itulie.
Wakati huo huo, baadhi ya meli kutoka Pakistan zimeendelea na safari kuelekea Falme za Kiarabu na Kuwait, zikionyesha kuwa si kampuni zote zimeamua kusitisha safari zao licha ya hatari inayoongezeka.
Kwa upande wake, jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran limeonya kuwa meli yoyote ya kijeshi itakayokaribia eneo hilo itachukuliwa kama kitendo cha uchokozi na itajibiwa kwa nguvu, hatua inayoongeza uwezekano wa kuzuka kwa mapigano mapya.

Athari kwa Uchumi wa Dunia
Mlango wa Strait of Hormuz ni njia muhimu inayopitisha sehemu kubwa ya mafuta duniani. Kuvurugika kwa usafiri katika eneo hilo kunaweza kusababisha:
- Kupanda kwa bei za mafuta kimataifa
- Kuongezeka kwa gharama za usafirishaji
- Shinikizo kwa uchumi wa nchi zinazoagiza mafuta kwa wingi
Wachambuzi wanaonya kuwa ikiwa hali itaendelea kuwa tete, dunia inaweza kushuhudia mshtuko mkubwa wa nishati ndani ya muda mfupi.