
Serikali ya Burundi imethibitisha kifo cha Waziri wa Mawasiliano na Vyombo vya Habari, Gabby Bugaga, kilichotokea Alhamisi asubuhi katika kile kilichoelezwa kuwa ajali, huku utata ukigubika mazingira ya kifo chake.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Serikali na Msemaji wa Serikali, Jerome Niyonzima, serikali imesikitishwa na kifo hicho cha ghafla kilichotokea alfajiri ya Alhamisi.
Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, naye ameonesha masikitiko yake kupitia mtandao wa X, akieleza kuwa taifa limepoteza kiongozi aliyekuwa na ujasiri, bidii na kujitolea katika kulitumikia.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa Bugaga alikutwa amefariki akiwa ndani ya gari dogo aina ya ‘pick up’ lililokuwa limeegeshwa katika shamba la michikichi eneo la Kivoga, kaskazini-magharibi mwa Jiji la Bujumbura, katika Wilaya ya Ntahangwa.
Hata hivyo, mazingira halisi ya ajali hiyo bado hayajabainishwa, na serikali haijaeleza aina ya ajali iliyotokea.
Wakati huo huo, video na picha ambazo hazijathibitishwa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilimuonesha marehemu akiwa ameegamia usukani ndani ya gari lililoharibika vibaya pembeni mwa barabara, jambo linalozua maswali zaidi kuhusu tukio hilo.

Bugaga, ambaye kabla ya kuingia serikalini alikuwa mwandishi wa habari, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Vyombo vya Habari mwezi Agosti 2025.
Kabla ya hapo, aliwahi pia kuwa mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Burundi akihusika na masuala ya lojistiki.
Serikali imeeleza kuwa taarifa zaidi kuhusu mazingira ya kifo hicho pamoja na mipango ya mazishi zitatolewa baadaye.