
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kutambua na kuheshimu mchango wa Mama Lishe na Baba Lishe katika maisha ya kila siku ya Watanzania, akieleza kuwa kundi hilo lina mchango mkubwa katika uchumi wa jamii na upatikanaji wa chakula kwa wananchi wengi.

Akizungumza katika Kongamano la Kitaifa la Mamalishe na Babalishe lililofanyika katika Julius Nyerere International Convention Centre jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema shughuli za kundi hilo zinapaswa kupewa hadhi na heshima inayostahili kutokana na umuhimu wake.

“Mtakubaliana nami kwamba shughuli za Mamalishe na Babalishe zinastahili kutambuliwa na kuheshimiwa kwa hadhi inayolingana na mchango wao katika maisha yetu ya kila siku. Yale yaliyosemwa hapa ya kunyanyaswa, ya kusumbuliwa, hayapaswi kufanywa kwa kundi hili,” alisema Rais Samia.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa utulivu, usalama na ufanisi zaidi. Pia amewataka viongozi katika maeneo mbalimbali nchini kuepuka vitendo vya unyanyasaji dhidi ya mama na baba lishe.

Rais Samia ameongeza kuwa kundi hilo ni sehemu muhimu ya mfumo wa chakula mijini na linachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa wananchi wa kipato cha chini, hivyo linapaswa kupewa kipaumbele katika sera na mipango ya maendeleo.
Kauli hiyo imeibua mjadala chanya kuhusu nafasi ya wafanyabiashara wadogo katika uchumi wa Tanzania na umuhimu wa kulinda haki zao katika mazingira ya kazi.
