
Serikali ya Zambia imethibitisha kuuchukua mwili wa Rais wa zamani Edgar Lungu aliyefariki dunia nchini Afrika Kusini miezi 10 iliyopita, hatua iliyozua mjadala mkubwa na mvutano mpya kati ya Serikali na familia yake.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Serikali imesema hatua hiyo inalenga kuandaa mazishi ya kitaifa kwa heshima ya Rais huyo wa zamani, ambaye anatarajiwa kuzikwa katika eneo maalum la viongozi wa kitaifa jijini Lusaka, sambamba na viongozi wengine waliowahi kushika wadhifa huo.
Hata hivyo, uamuzi huo umepingwa vikali na familia ya marehemu, ambayo imeendelea kusisitiza kuwa inataka mazishi ya kifamilia na ya faragha, bila kuingiliwa na Serikali.
Mvutano huo wa muda mrefu kati ya familia na Serikali ulifikishwa katika mahakama za Afrika Kusini, ambapo Mahakama iliruhusu mwili huo kurejeshwa Zambia kwa ajili ya mazishi ya kitaifa, ingawa familia iliendelea kupinga kupitia rufaa.
Serikali ya Zambia imesema kuchukua mwili huo kumekuja baada ya kile ilichodai kuwa kushindwa kwa familia kuendelea na taratibu za kisheria kwa wakati uliopangwa, hatua ambayo imezidisha hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wa mazishi hayo.
Kwa upande mwingine, mawakili wa familia ya Lungu wamewasilisha ombi la dharura katika Mahakama Kuu ya Afrika Kusini wakitaka mwili huo urejeshwe katika chumba cha kuhifadhia maiti ulikokuwa awali, wakisisitiza kuwa haki za familia zinapaswa kuheshimiwa.
Sakata hilo linaendelea kufuatiliwa kwa karibu huku likizua mjadala mpana kuhusu mila, heshima za kitaifa na haki za familia katika mazishi ya viongozi wa juu wa taifa.