
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ametangaza kuanza ziara muhimu ya kidiplomasia katika nchi tatu Pakistan, Russia na Oman akiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na kujadili hali ya kisiasa katika eneo hilo.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Araghchi alisema kuwa ziara hiyo inalenga kuhakikisha Iran inashirikiana kwa karibu na washirika wake wa kikanda. “Majirani zetu ni kipaumbele chetu,” alisisitiza.
Ziara hii inakuja wakati ambapo mvutano kati ya Iran na Marekani bado upo juu, licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda. Hata hivyo, jitihada za kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili zinaonekana kukwama baada ya duru ya pili ya mazungumzo iliyopangwa kufanyika Islamabad, Pakistan, kushindikana.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, ujumbe wa Marekani uliokuwa ukiongozwa na Makamu wa Rais JD Vance haukusafiri kwenda Pakistan kama ilivyotarajiwa. Sababu kuu ya kusitishwa kwa mazungumzo hayo inadaiwa kuwa ni msimamo wa Iran kukataa kushiriki mazungumzo ya ana kwa ana hadi Marekani itakapositisha vikwazo vyake vya kiuchumi.
Katika duru ya kwanza ya mazungumzo iliyofanyika mapema mwezi huu nchini Pakistan, maafisa wa juu wa Marekani, akiwemo mjumbe maalum Steve Witkoff na Jared Kushner, walikutana na wajumbe wa Iran, lakini hakuna makubaliano yaliyofikiwa.
Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth alitoa kauli kali akisema Iran ina nafasi ya kufikia makubaliano, lakini akaonya kuwa Marekani iko tayari kwa hatua zozote zitakazofuata iwapo mazungumzo yatashindikana.