×

Influencer Klaudiaglam Afariki Baada ya Kugongwa na Gari London

Mrembo maarufu wa mitandaoni na Influencer, anayejulikana kama Klaudiaglam (jina halisi Klaudia Zakrzewska) amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 32, baada ya kujeruhiwa vibaya katika tukio la kugongwa na gari lililoripotiwa kuhusisha mshawishi mwingine wa mitandaoni mjini London.

Kwa mujibu wa taarifa za Polisi wa Metropolitan wa London, tukio hilo lilitokea Aprili 19 katika eneo la Argyll Street, ambapo Zakrzewska aligongwa na gari na kupelekwa hospitalini akiwa katika hali mahututi. Baada ya siku kadhaa akiwa chini ya uangalizi, alitangazwa kufariki dunia Aprili 25.

Polisi wamesema mshukiwa katika tukio hilo ni Gabrielle Carrington, anayejulikana mtandaoni kama RielleUK, ambaye awali alikuwa ameshtakiwa kwa jaribio la mauaji. Kufuatia kifo cha Zakrzewska, mashitaka hayo sasa yanatarajiwa kubadilishwa kuwa mauaji (murder).

Taarifa za awali za uchunguzi zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea baada ya mzozo uliodaiwa kuhusisha watu hao wawili, ambapo kamera za CCTV zilionyesha gari likienda kwa kasi kuelekea mhanga kabla ya kumgonga.

Katika tukio hilo, mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 58 pia alijeruhiwa vibaya na kuathiriwa maisha yake kwa muda mrefu.

Mpelelezi mkuu wa kesi hiyo, DCI Alison Foxwell, alisema:
“Tunatoa rambirambi zetu kwa familia na marafiki wa Klaudia. Pia tunawasihi watu kuepuka kusambaza video au picha za tukio hilo ambazo zinaweza kuathiri uchunguzi unaoendelea.”

Polisi pia wamethibitisha kuwa uchunguzi bado unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo pamoja na mazingira yaliyopelekea mzozo huo.

Wote wawili, Zakrzewska na Carrington, walijulikana mtandaoni kwa kushiriki maudhui ya mitindo ya maisha, mitindo ya mavazi na safari zao mbalimbali za kimataifa kabla ya tukio hilo la kusikitisha.

TRUMP AACHIA VIDEO za CCTV WAKATI MSHUKIWA AKIFYATUA RISASI – ALIVYOPAMBANA na WALINZI 📍USA

Leave a Comment