
Rais wa Marekani, Donald Trump, aliondolewa kwa dharura na maafisa wa usalama baada ya milio ya risasi kusikika wakati wa hafla ya kila mwaka ya White House Correspondents’ Dinner iliyokuwa ikiendelea jijini Washington.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 2:30 usiku kwa saa za Marekani, ambapo wageni walilazimika kukimbia na kujificha chini ya meza kufuatia taharuki iliyosababishwa na milio ya risasi. Trump pamoja na mkewe, Melania Trump, walitolewa haraka ukumbini na maafisa wa Secret Service.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Trump alisema hakutambua mara moja kilichokuwa kinaendelea.
“Nilisikia kelele, nikadhani labda ni sahani imeanguka… lakini ilikuwa ni bunduki,” alisema.
Aliongeza kuwa wakati wa tukio hilo alikuwa mbali na eneo lilipotokea shambulio na mshukiwa hakufanikiwa kukaribia eneo alilokuwepo. Hata hivyo, alikiri kuwa uongozi ni kazi yenye hatari kubwa akisema, “Ni kazi hatari.”
Mshukiwa wa tukio hilo ametambuliwa na vyombo vya usalama kama kijana mwenye umri wa miaka 31 kutoka California, ambaye kwa sasa yuko chini ya ulinzi huku akipatiwa matibabu. Kwa mujibu wa taarifa za awali, mshukiwa huyo alikuwa na silaha mbili shotgun na bastola wakati wa tukio.
Todd Blanche alisema uchunguzi unaendelea na hatua za kisheria zinatarajiwa kuchukuliwa hivi karibuni.
Katika tukio hilo, askari mmoja wa Secret Service alijeruhiwa baada ya kupigwa risasi, lakini aliokolewa na koti maalum la kuzuia risasi (bulletproof vest). Trump alisema alizungumza na askari huyo na kumkuta akiwa katika hali nzuri.
Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi, mshukiwa alidai kuwa lengo lake lilikuwa kuwashambulia maafisa wa serikali ya Trump, ingawa hakubainisha moja kwa moja kumlenga rais mwenyewe.
Licha ya tukio hilo, Trump alisifu mshikamano ulioonyeshwa ndani ya ukumbi huo, akisema watu wa makundi tofauti ya kisiasa walionekana kuwa kitu kimoja wakati wa taharuki hiyo.
“Huu ulikuwa usiku uliokusudiwa kusherehekea uhuru wa kujieleza, na kwa namna fulani uliwaunganisha watu,” alisema.
Hafla hiyo imeahirishwa na inatarajiwa kufanyika tena ndani ya siku 30 zijazo, huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.