
Mfanyabiashara mkazi wa Kigamboni, Rehema Maulid Hassan (42), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka moja la mauaji ya mtayarishaji wa filamu, Athuman Nyanza.
Mshtakiwa amesomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Mswalo, kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Florida Wencelaus, ambaye ameeleza kuwa mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji kwa hatua hiyo.
Upande wa mashtaka umedai kuwa Rehema anashtakiwa kwa kosa la mauaji, kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2013.
Inadaiwa kuwa Februari 10, 2026, katika eneo la Mwapemba, Kigamboni jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alimuua Athuman Said Nyanza.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Mswalo ameeleza kuwa mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Upande wa Jamhuri umedai kuwa upelelezi bado unaendelea.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 13, 2026, huku mshtakiwa akiendelea kubaki mahabusu kwa kuwa kosa hilo halina dhamana.
🔴 Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.