
Mkuu wa Idara ya Habari wa Simba, Ahmed Ally leo Mei 1, 2026 amezungumzia viingilio vya mechi ya Kariakoo Dabi utakaofanyika Mei 3, 2026, katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, akisema kwamba viingilio vimewekwa kwa bei rafiki ili kila Mwanasimba aweze kushiriki katika mechi hiyo muhimu.
Alisema, “Hatujataka kuweka viingilio vya kausha damu ili kila Mwanasimba aweze kuingia. Kwa uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo tungeweka viingilio vikubwa, lakini tumeweka viingilio rafiki.”
Viingilio vya mechi hiyo ni Tsh 15,000 kwa Mzunguko, Tsh 30,000 kwa VIP B, na Tsh 50,000 kwa VIP A. Semaji alisisitiza kwamba tiketi zimeanza kuuzwa na akawataka mashabiki wanunue tiketi mapema, kwani tiketi zitakuwa chache na zitauzwa haraka.
“Ukisema nitanunua kesho, nawahakikishia mpaka kesho muda huu tiketi hazitakuwepo,” aliongeza.
Aidha, alizungumzia juhudi zinazochukuliwa kudhibiti wizi wa tiketi na vishoka. “Tumezungumza na N-Card kuangalia namna ya kudhibiti vishoka ili asije kutuharibia mechi yetu. Yupo mtu ambaye jana ametaka kununua tiketi robo tatu ya uwanja, anataka kupeleka wapi hatujui.”
Kwa mashabiki watakaokosa tiketi, Semaji alisema kwamba wataweza kufuata mechi hiyo kupitia Azam TV ambayo itarusha mechi hiyo moja kwa moja. “Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo tunatarajia utaingiza mashabiki 10,000 na kama hutapata tiketi tafadhali baki nyumbani kwako.”
Alimalizia kwa kusema, “Eneo lile lote na uwanja lipo chini ya JKT. Kama huna tiketi kaa mbali, Azam TV itakusaidia kuangalia live. Kama huna tiketi na unatokea Dar mwisho wako Kunduchi, kama unatokea Bagamoyo mwisho wako Mapinga.”