
Rais wa Marekani Donald Trump amesema hajaridhishwa na pendekezo jipya la Iran la kumaliza vita kati ya mataifa hayo mawili, akieleza pia kuwa uongozi wa Iran “umegawanyika.”
Akizungumza Ijumaa katika Ikulu ya White House, Trump alisema alilikataa pendekezo hilo mara baada ya kuwasilishwa kupitia wapatanishi nchini Pakistan.
“Wanataka makubaliano, lakini sijaridhika nayo. Tutaona kitakachotokea,” alisema, bila kueleza mapungufu aliyoyaona katika mpango huo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran IRNA, pendekezo hilo liliwasilishwa kwa wapatanishi Alhamisi usiku.
Licha ya kuwepo kwa usitishaji mapigano wa takriban wiki tatu, hali bado ni tete huku Marekani na Iran zikishutumiana kwa kukiuka makubaliano.
Mvutano mkubwa unaendelea katika Mlango wa Strait of Hormuz, ambapo takriban 20% ya mafuta na gesi duniani hupita. Marekani imeweka mzingiro wa kijeshi kuzuia meli za Iran, hali inayodhoofisha uchumi wa Iran na kuongeza presha kwa uchumi wa dunia.
Trump alisema mazungumzo bado yanaendelea kwa njia ya simu baada ya kufuta safari ya wajumbe wake kwenda Pakistan. Pia alidokeza mpango mpya wa kufungua tena njia hiyo muhimu kwa usafirishaji wa mafuta.
Hata hivyo, alionesha kuchoshwa na uongozi wa Iran.
“Uongozi wao haujaungana. Wote wanataka makubaliano, lakini hawako sawa,” alisema.
Trump aliongeza kuwa Marekani ina chaguzi mbili tu: Kuendelea na mashambulizi makali ya kijeshi au kufikia makubaliano ya kidiplomasia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alifanya mawasiliano na nchi kadhaa za kikanda ikiwemo Uturuki, Misri, Qatar na Saudi Arabia, akieleza juhudi za kumaliza vita.
Pia alizungumza na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, kuhusu njia za kufungua tena mlango wa Hormuz na kuhakikisha usalama wa muda mrefu.