
Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Yashiriki Mazungumzo ya Kuimarisha Kilimo na Biashara ya Kikanda katika Jukwaa la Uchumi la Tanzania–Kenya
Dar es Salaam, 4 Mei 2026: Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imekuwa miongoni mwa wadau wa sekta binafsi walioshiriki katika Jukwaa la Uchumi la Tanzania na Kenya, lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, likileta pamoja viongozi wa serikali, wawekezaji na taasisi mbalimbali kujadili fursa za kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Jukwaa hilo, lililofanyika kama sehemu ya ziara ya Kiserikali ya Rais wa Kenya Mheshimiwa, Daktari William Samoei Ruti na Mwenyeji wake Mheshimiwa, Daktari Samia Suluhu Hassan, liliangazia namna ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, biashara, nishati, utalii na huduma za kifedha.
Kwa sasa, biashara kati ya Tanzania na Kenya imevuka dola za Marekani bilioni 1, ikiashiria ukuaji wa mahusiano ya kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
Akichangia katika mjadala kuhusu Kilimo, Biashara na Uwekezaji, Kutoka Shambani hadi Sokoni, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Dk. Obinna Anyalebechi, alieleza uzoefu wa kampuni hiyo katika kujenga mnyororo wa thamani wa kilimo kupitia ushirikiano na wakulima wa ndani.
“SBL ni kampuni ya Kitanzania, na kwa miaka mingi tumewekeza katika kilimo kama sehemu ya msingi ya biashara yetu. Leo, zaidi ya asilimia 80 ya malighafi tunazotumia zinatoka ndani ya nchi, kupitia ushirikiano na wakulima wadogo,” alisema.
Aliongeza kuwa uzoefu huo unaonesha kwa vitendo namna sekta binafsi inavyoweza kuchangia katika kuimarisha uzalishaji wa ndani na kufungua fursa za kiuchumi kwa wakulima.
Kupitia programu ya Shamba ni Mali, SBL inafanya kazi na zaidi ya wakulima wadogo 600 nchini, huku ikinunua mazao ya ndani kama mtama, mahindi na shayiri. Katika mwaka 2024, kampuni ilinunua zaidi ya tani 20,000 za mazao hayo, na kuchangia takribani shilingi za Kitanzania bilioni 12 moja kwa moja katika minyororo ya thamani ya wakulima.
Katika mjadala huo, wadau mbalimbali walisisitiza umuhimu wa kuimarisha mazingira ya uwekezaji, ikiwemo sera thabiti, miundombinu rafiki ya biashara ya mipakani, na ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi ili kufungua fursa zaidi katika sekta ya kilimo.
Aidha, kulijadiliwa nafasi ya teknolojia ya kidijitali katika kuunganisha masoko, kuongeza uwazi katika uzalishaji na kusaidia wakulima kupata huduma za kifedha pamoja na taarifa muhimu za uzalishaji.
Jukwaa hilo pia lilitoa msisitizo juu ya haja ya kuondoa vikwazo visivyo vya kodi (non-tariff barriers) ili kurahisisha biashara ya bidhaa, hasa za kilimo, kati ya Tanzania na Kenya.
Kama sehemu ya ushiriki wake, SBL iliungana na wadau wengine wa sekta binafsi katika shughuli za mawasiliano na majadiliano ya pembeni, ikiwa ni pamoja na hafla ya kukutanisha wadau iliyolenga kuimarisha mahusiano na kubadilishana uzoefu.
Akihitimisha, Dk. Anyalebechi alibainisha kuwa ushirikiano wa kikanda una nafasi kubwa katika kukuza uchumi jumuishi:
“Tanzania na Kenya zina nafasi ya kukua pamoja. Kupitia ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi, tunaweza kujenga mfumo imara wa kilimo na biashara unaowanufaisha wakulima, wawekezaji na uchumi wa kanda nzima.”