
Kilwa, Lindi – Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania, kwa kushirikiana na Bilal Muslim Mission of Tanzania pamoja na KSI Charitable Centre, imeendesha kambi ya siku tatu ya huduma za macho bure kwa wananchi wa Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.
Kupitia kambi hiyo, mamia ya wananchi walipata huduma mbalimbali ikiwemo vipimo vya macho, matibabu pamoja na upasuaji wa macho uliotekelezwa na madaktari bingwa. Lengo la mpango huo ni kusaidia jamii kupata huduma za afya ya macho kwa urahisi, hususan kwa wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Akifungua rasmi kambi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo, aliwataka wazazi kuchukua hatua za haraka wanapobaini dalili za matatizo ya macho kwa watoto wao kwa kuwapeleka hospitali mapema ili kuepusha madhara makubwa zaidi.

Alitoa wito huo kufuatia kubainika kuwepo kwa baadhi ya watoto wenye umri wa miaka minane waliofika katika kambi hiyo wakiwa tayari na changamoto kubwa za macho, hali iliyosababisha madaktari kueleza kuwa huenda baadhi yao wamechelewa kupata matibabu sahihi kwa wakati.
Akizungumzia mpango huo, Mkuu wa Yas Kanda ya Pwani Kusini, Bi. Fadhila Saidi, alisema: “Yas Tanzania tunaamini kuwa afya bora ni msingi wa maendeleo ya jamii. Kupitia ushirikiano huu, tumedhamiria kuleta huduma za macho karibu zaidi na wananchi, hasa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa kama Kilwa. Tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha jamii inanufaika na huduma muhimu za afya.”

Kwa upande wake, Mratibu wa kambi hiyo kutoka Bilal Muslim Mission of Tanzania, Ain Sharif, alisema huduma zinazotolewa ni pana na zinalenga kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu kamili kwa wakati.
Alisema: “Huduma hizi za bure zinajumuisha uchunguzi wa macho, utoaji wa dawa na miwani kwa waliokutwa na tatizo, ushauri wa kitaalamu pamoja na upasuaji mdogo wa mtoto wa jicho kwa wagonjwa watakaobainika kuwa na tatizo hilo. Wagonjwa watakaohitaji matibabu ya juu zaidi watapewa rufaa ili waendelee kupata huduma katika vituo vyenye uwezo mkubwa.”
Yas Tanzania imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kurejesha kwa jamii na kuimarisha ustawi wa wananchi.