
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amehitimisha mgogoro wa nyumba uliopo eneo la Mikocheni, kiwanja namba 317 Regent Estate, ambapo amesema kuwa kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, nyumba hiyo ni mali ya Godifrey Shuma na Carista Shuma. Aidha, amemtaka Bi Everlin Chiomba, aliyekuwa akiishi hapo akidai nyumba hiyo ni mali yake aliyorithi kutoka kwa marehemu mumewe, kuondoka kwenye nyumba hiyo ndani ya muda wa saa moja na nusu.
Akizungumza katika mtaa wa Regent, eneo la Mikocheni, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila amesema Godifrey Shuma na Carista Shuma ndio wamiliki halali wa nyumba hiyo kwa mujibu wa maelekezo ya mahakama na nyaraka zilizopo. Hivyo, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni pamoja na RPC wa Kinondoni kusimamia zoezi hilo ili mwenye haki akabidhiwe nyumba hiyo, huku akimtaka Bi Everlin Chiomba kurejea mahakamani endapo hataridhika na maamuzi hayo.

RC Chalamila ameongeza kuwa yupo tayari kumsaidia Bi Everlin Chiomba kurejea mahakamani ili kupata ufafanuzi zaidi na ushauri wa kitaalamu. Hata hivyo, amesema kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, mmiliki halali ni Godifrey Shuma na Carista Shuma. Pia ameitaka Ofisi ya Ardhi na Mahakama kumsaidia kumaliza kitendawili cha binti aliyejitokeza akidai kuwa ni mtoto wa marehemu Chiomba, aliyekuwa mmiliki wa awali wa nyumba hiyo. Inadaiwa mtoto huyo anatumia majina mawili tofauti, Flora Chiomba na Flora Mwashaa.
Aidha, kabla ya uamuzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliunda kamati ya kufuatilia suala hilo. Mwenyekiti wa kamati hiyo ya mgogoro, Mbaraka Forogo, alipowasilisha taarifa yake alisema kamati imejiridhisha kuwa nyumba hiyo iliuzwa na kwamba Godifrey Shuma ndiye mwenye hati miliki ya sasa.
Vilevile, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amekemea kitendo kilichofanywa na mtoto anayedai ni wa marehemu Chiomba, Bi Flora, kwa kuleta mabaunsa kufanya fujo, wakati tayari matumizi ya mabaunsa yalishapigwa marufuku.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukrani Kyando, ameeleza kuwa Godifrey Shuma na Carista Shuma ndio wamiliki halali wa nyumba hiyo kwa mujibu wa nyaraka.