
Washington, Marekani – Kauli tata kuhusu madai ya matumizi ya Dolphin wa kujitoa muhanga katika shughuli za kijeshi za Iran imezua mjadala mkubwa wa kimataifa, huku Marekani ikikanusha uwepo wa taarifa hizo.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Idara ya Ulinzi ya Marekani, Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth aliulizwa kuhusu ripoti zilizosambaa zikidai kuwa Iran inaweza kutumia wanyama wa baharini, wakiwemo dolphins, katika mashambulizi dhidi ya meli za kivita za Marekani.
Akijibu swali hilo, Hegseth alisema hawezi kuthibitisha wala kukanusha uwepo wa Dolphin wa kujitoa muhanga, lakini akasisitiza kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa Iran inamiliki au inatumia wanyama hao kwa shughuli za kijeshi.
“Sina uhakika kuhusu kamikaze dolphins, lakini naweza kuthibitisha kuwa Iran haina hizo,” alisema kwa ufupi, kauli iliyozua mijadala zaidi kwenye mitandao ya kijamii.
Ripoti za awali zilichapishwa na gazeti la The Wall Street Journal, zikidai kwa kunukuu maafisa wa Iran kuwa Tehran inaweza kutumia silaha zisizotarajiwa dhidi ya meli za Marekani, ikiwemo manowari na hata wanyama wa baharini wanaobeba vilipuzi.
Tangu ripoti hizo zianze kusambaa, vyombo mbalimbali vya habari nchini Marekani, ikiwemo CNN na Fox News, vimekuwa vikichambua madai hayo, huku yakipokelewa kwa mashaka na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kijeshi.
Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari nchini Iran vimeyataja madai hayo kuwa ya kushangaza na yasiyo na msingi, huku yakionekana zaidi kama taarifa za kimtandao au kejeli za kisiasa.
Ubalozi wa Iran katika mji wa Hyderabad, India, pia ulisambaza picha iliyotengenezwa kwa akili mnemba (AI) ikimuonyesha dolphin akiwa na kifaa kinachofanana na mlipuko kilichofungwa mwilini, pamoja na ujumbe uliosema kuwa siri zote zimefichuliwa,” hatua iliyoongeza utata zaidi kuhusu madai hayo.
Kwa upande mwingine, Marekani inaendelea kuwa na mpango rasmi wa kijeshi unaojulikana kama US Navy Marine Mammal Program, unaotumia wanyama kama dolphins na sea lions kusaidia kugundua mabomu ya baharini na vitu hatarishi chini ya maji.
Mpango huo, hata hivyo, unalenga kazi za ulinzi na uokoaji pekee, na si matumizi ya mashambulizi ya kivita.