
Zaidi ya meli 1,600 zimeendelea kusalia karibu na mlango wa bahari wa Strait of Hormuz huku hali ya usalama ikizidi kuwa tete kutokana na mvutano wa kivita unaoendelea katika eneo hilo.
Kampuni nyingi za usafirishaji wa baharini zimeonekana kuwa na tahadhari kubwa kuhusu kuruhusu meli zao kuendelea na safari, zikihofia mashambulizi yanayoweza kuhatarisha maisha ya wafanyakazi pamoja na kusababisha hasara kubwa ya mali na mizigo.
Ripoti zinaeleza kuwa jitihada za muda mfupi za Marekani kusaidia kusindikiza baadhi ya meli kupita salama katika eneo hilo hazikutoa suluhisho la kudumu, kwani operesheni hiyo ilidumu kwa saa 48 pekee na meli mbili tu zikafaidika.

Wataalamu wa sekta ya usafirishaji wanaeleza kuwa kampuni nyingi sasa zinafanya tathmini ya kina kabla ya kuchukua hatua yoyote, hasa kutokana na gharama kubwa zinazoweza kutokea endapo meli zitaharibiwa wakati wa mashambulizi.
Pia imeelezwa kuwa baadhi ya kampuni za bima zina masharti maalum yanayohusiana na vita, hali inayoweza kufanya kampuni za meli kubeba hasara zenyewe endapo kutatokea mashambulizi.
Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) limesema tangu kuanza kwa mvutano huo, meli kadhaa tayari zimeshambuliwa kwa makombora na kusababisha vifo pamoja na majeruhi.
Kutokana na hali hiyo, IMO imezitaka meli zote kuwa makini zaidi wakati wa kupita katika eneo hilo huku ikionya kuwa ulinzi wa kijeshi wa kusindikiza meli hauwezi kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto hiyo.
