
Raia wa China Xu Fuyu mwenye umri wa miaka 39 na mfanyakazi wake wa mgahawa wa Kibonge uliopo Kariakoo Dar esSalaam, Blandina Mwalutola mwenye miaka 24 wamehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni sita au kifungo cha miaka mitatu jela kwa kushindwa kutoa risiti ya kielektroniki, baada ya kutoa huduma ya chipsi kuku, sahani ya baga, sahani ya wali na vinywaji
Aidha, imedaiwa kuwa washtakiwa hao walikamatwa, wakati maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakiwa katika utafiti na upelelezi kuhusianana na utoaji wa risiti za kielektroniki, waliagiza chakula na vinywaji ila walipewa risiti za mkono.
Washtakiwa wote wameshtakiwa Kinyume na Kifungu cha 97(1)(b) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi [Sura ya 438 Toleo la 2023], kikisomwa pamoja na Vifungu vya 96 na 97 vya Sheria ya Fedha Na. 6 ya mwaka 2024.
Hukumu hiyo, imetolewa Mei 08, 2026 na Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya Ilala Dar es Salaam Mhe. Mohamed Burhani, baada ya washtakiwa kukiri mashtaka mawili kushindwa kutoa risiti za kielektroniki kinyume na sheria za kodi.
Hakimu Burhani alisema kesi kama hizo lazima adhabu zitolewe ili kuzuia makosa hayo yasitendwe na watu wengine.
“Kwa mujibu wa sheria sitawapa adhabu ya Magereza nitawaacha huru iwapo mtalipa faini kwa sababu mmekiri mashtaka yenu, shtaka la kwanza kila mmoja atalipa faini ya Sh milioni mbili na shtaka la pili ambalo linamkabili Fuyu peke yake atalipa Sh milioni mbili,” alisema Hakimu Burhani
Hata hivyo, Hakimu Burhani aliwaeleza washtakiwa kuwa wakishindwa kulipa faini hiyo kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela, ambapo waliweza kulipa faini hiyo na kuachiwa huru.
Awali, Wakili wa Serikali Salome Assey akisoma hati ya mashtaka, alidai kuwa washtakiwa hao Machi 24, 2026 katika Mtaa wa Gerezani, eneo la Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watoa huduma za chakula na vinywaji katika Kampuni ya Dicos (Mgahawa wa Kibonge), walishindwa kutoa risiti ya kielektroniki walipotoa huduma ya chakula ambayo ni sahani moja ya baga yenye thamani ya Sh.13,000.
Katika shtaka la pili, inadaiwa kuwa tarehe hiyo na mahali hapo mshtakiwa Fuyu alishindwa kutoa risiti ya kielektroniki alipotoa huduma ya chakula na vinywaji ambayo ni sahani mbili za chipsi kuku, sahani moja ya wali uliochanganywa na mayai, chupa mbili za plastiki za Coca-Cola na chupa moja ya maji ya kunywa ya Kilimanjaro, vyote vikiwa na thamani ya Shilingi 35,000.
Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka hayo, walikiri kutenda makosa hayo ambayo Hakimu Burhani aliutaka upande wa mashtaka kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali (PH).
Alidai kuwa Machi 24,2026 Fuyu akiwa Meneja wa Kampuni hiyo na Mwalutola akiwa mhudumu walikuwa wanatoa huduma ya chakula na vinywaji kwa wateja na tarehe maofisa wa TRA walipewa kazi kwa ajili ya kufanya utafiti na upelelezi katika mgawaha huo kama wanatoa risiti za kielektroniki.
Ilidaiwa kuwa Ofisa wa TRA, Cecilia Lussa aliagiza sahani ya baga ambayo ilikuwa ni Sh. 13,000 na baada ya kulipa fedha alipewa risiti ya mkono, alipouliza kwa nini hajapewa risiti ya kielektroniki aliambiwa mashine haifanyi kazi ni mbovu.
“Na maofisa wengine wawili Hosea Kasiba na Kisabo Focus walifika katika mgawaha huo, wakaagiza sahani mbili za chipsi kuku, sahani moja ya wali iliyochanganywa na mayai, chupa mbili za Coca-Cola na maji ya Kilimanjaro chupa mbili jumla ilikuwa Sh 35,000, baada ya kulipa walipewa risiti ya mkono, walipouliza walielezwa kuwa mashine ni mbovu,”alidai
Baada ya hapo walijitangaza kama wao ni maofisa wa TRA, watuhumiwa walikwenda kuripoti Idara ya Kodi kwa kosa la kushindwa kutoa risiti za kielektroniki , ambapo walikiri kutenda kosa hilo.
Hata hivyo, washtakiwa walikili maelezo hayo kuwa ni ya kweli, Mahakama ilipokea vielelezo mbalimbali vya Jamhuri ikiwemo risiti walizozitoa kwa wateja kama kielelezo namba moja.
“Baada ya kusomewa mashtaka yenu mmekiri kosa hilo na PH pia mmekiri kutokana na kukiri kwenu Mahakama inawatia hatiani kwa makosa yote. Je! Jamhuri washtakiwa wanamakosa ya nyuma?,”alisema Hakimu Burhani
Hata hivyo, Wakili Assey alidai hawana taarifa za nyuma za washtakiwa, kwa hiyo hakimu aliwapa nafasi ya washtakiwa kujitetea kabla adhabu haijatolewa.
Fuyu ambaye ni Meneja Kampuni ya Decos Catering Ltd na Mkazi wa GSM Plaza -Gerezani amedai kuwa yeye ni bosi na pia ni mpishi kwa wakati mmoja, kwa hiyo hawezi kuona kinachoendelea kama risiti za kielektroniki zinatolewa au, ila anakubali kutenda kosa hilo.
Mshtakiwa wa pili, Mwalutola ambaye ni Mkazi wa Temeke Mwembe Yanga alidai kuwa siku hiyo kweli mashine ilikuwa inasumbua ilikuwa ikiandika ‘Illegal’, lakini ilipotengemaa waliendelea kutoa risiti za kielektroniki kwa sababu ndiyo utaratibu wao ni siku hiyo tu ndiyo kulitokea changamoto.
Wakati kesi hiyo inaendelea, Mkalimani Maria Katambo alikuwa akitafsiri kutoka lugha ya kiswahili kwenda Kichina na kichina kwenda Kiswahili kwa ajili ya mshtakiwa Fuyu na alipewa ruhusa hiyo na mahakama baada ya kula kiapo.