
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesifu mchango mkubwa wa Oryx Energies katika sekta ya nishati nchini huku pia ikifurahishwa na utoaji wa ajira kwa Watanzania kwa asilima 90.
Aidha kamati hiyo imesema pia inatambua mchango wa kampuni hiyo katika kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Ssmia Suluhu Hassan katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia nchini ambapo katika kipindi kifupi watumiaji wa nishati hiyo wameongezeka kutoka asilimia 6 mpaka 27 na Oryx amekuwa mdau muhimu katika ongezeko hilo.
Kamati hiyo ya Bunge imefanya ziara maalum katika Kampuni ya Oryx Energies leo Mei 9,2026 jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na kupokea taarifa imeshuhudia uwekezaji mkubwa uliofanywa katika kiwanda cha kisasa cha kutengeneza vilainishi kilichopo Kurasini pamoja na kiwanda cha Oryx Gas kilichopo Kogambani ,Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge -Nishati na Madini Subira Mgau amesema uwekezaji uliofanyika na kampuni hiyo ni uthibitisho wa namna ambavyo Serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira mazuri ya kuwa na uwekezaji wenye tija.
Amefafanua hata Dira ya 2050 ambayo imeanza kutekelezwa na mpango wa miaka mitano ambapo sekta binafsi inategemewa kwa asilimia 70 na uwekezaji wa Oryx Energies ni muhimu katika kufikiwa kwa malengo ya serikali kupitia dira hiyo.

Ameongeza pia kamati hiyo wameona mchango wa kampuni hiyo katika pato la Taifa kupitia kodi ambapo taarifa yao inaonesha wamechangia Sh.Trilioni 1.2 kupitia kodi na michango mbalimbali huku pia akielezea ajira walizotoa kwa Watanzania kwa zaidi ya asilimia 90.
Kuhusu nishati safi ya kupikia kamati imeipongeza Oryx Gas Tanzania kwa hatua mbalimbali inazochukua kuhamasisha nishati hiyo nchini huku pia ikioneshwa kufurahishwa na mkakati wa kampuni hiyo kwani pamoja na vita vinavyoendelea lakini wao wamethihitisha upatikanaji wa gesi ya kupikia majumbani ni wa uhakika.
Awali akitoa Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania Limited Imani Mtafya amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kampuni hiyo ya Oryx Energies imewekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 10 katika kiwanda cha kutengeneza vilainishi huku pia wakihakikisha wanatoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 99.

Aidha amesema Oryx Energies inafanya kazi kubwa nne ,ambazo ni kusambaza na kuuza gesi , kuuza mafuta ya dizeli na petroli pamoja na vilainishi ambapo wao ndio wazalishaji wakubwa kwa Afrika Mashariki.
Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amewahakikishia Wabunge kupitia Kamati hiyo kuwa kampuni hiyo imejipanga kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia sambamba kuwatoa
hofu wabunge kuwa nishati safi ya kupikia ipo ya kutosha.
Pia amesema kwa sasa Oryx Gas inatekeleza upanuzi mkubwa ghala la kupokea na kuhifhadhi gesi ya LPG eneo la Kigamboni ambapo mradi huo utawezesha kampuni kupokea LPG kwa wingi, kuhakikisha upatikanaji wa kutosha nchini Tanzania huku ukipunguza gharama za usambazaji na kuongeza ufanisi.
Hata hivyo wabunge wa kamati hiyo wakiwa katika Kampuni ya Oryx Gas Tanzania wameshuhudia ubora wa hali ya juu wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.