×

Siku ya Mama Duniani: David Kafuila Atoa Ujumbe Kuhusu Siku 1000 za Maisha ya Mtoto

Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafuila.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafuila ametoa ujumbe maalum wa maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani, akisisitiza umuhimu wa malezi bora kwa watoto kuanzia siku za mwanzo za maisha.

Kafuila amesema kipindi cha siku 1,000 za mwanzo wa maisha ya mtoto, kuanzia mimba hadi kufikisha umri wa miaka miwili, kina nafasi kubwa katika kuamua ubora wa afya, ukuaji wa akili na maendeleo ya baadaye ya mtoto.

Ameeleza kuwa uwekezaji katika kipindi hicho ni msingi muhimu wa kujenga rasilimali watu bora, akibainisha kuwa ndicho kipindi kinachoweza kuzuia changamoto ya udumavu wa akili na kimwili kwa watoto, changamoto ambayo bado ni kubwa katika bara la Afrika.

Akizungumza zaidi, David Kafuila amesema kufikia Dira ya Maendeleo ya 2050, ubora wa rasilimali watu ndio nguzo kuu ya maendeleo endelevu, na hivyo jamii inapaswa kuwekeza zaidi katika afya na lishe bora kwa watoto katika hatua za awali za maisha yao.

Akinukuu tafiti za Benki ya Dunia, Kafuila amesema uwekezaji sahihi katika siku 1,000 za mwanzo kwa mtoto wa Afrika unaweza kuongeza zaidi ya dola trilioni 3.8 katika uchumi wa dunia ifikapo mwaka 2035, kupitia nguvu kazi yenye tija na afya bora.

Aidha, amewapongeza akina mama duniani kote kwa mchango wao mkubwa katika malezi ya familia na maendeleo ya jamii, licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika maisha ya kila siku.

Amehitimisha ujumbe wake kwa kuwatakia heri akina mama wote duniani, hususan akina mama wa Afrika, akisisitiza kuwa wao ndio msingi wa kizazi cha baadaye na injini ya maendeleo ya jamii.

“HAPPY MOTHER’S DAY,” ameandika David Kafuila katika ujumbe wake.

MTANZANIA ALIYEISHI MIAKA 8 OMAN ANAFICHUA MAZITO – PESA ALIZOINGIZA HADI MAFANIKIO MAKUBWA

Leave a Comment