
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa anafikiria uwezekano wa kuifanya Venezuela kuwa jimbo la 51 la Marekani, hatua ambayo imezua mjadala mkubwa kimataifa kuhusu mustakabali wa taifa hilo la Amerika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya Marekani, Trump alitoa kauli hiyo katika mahojiano na kituo cha habari cha Fox News, akieleza kuwa uhusiano kati ya Marekani na Venezuela umeimarika baada ya operesheni ya kijeshi iliyompelekea kukamatwa kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Nicolas Maduro.
Trump amesema Venezuela kwa sasa inaendeshwa vizuri na uzalishaji wa mafuta umeongezeka kwa kiwango kikubwa huku kampuni kubwa za mafuta kutoka Marekani zikianza kuwekeza nchini humo.

Kauli hiyo imekuja miezi michache baada ya Marekani kufungua tena ubalozi wake mjini Caracas na kurejesha safari za ndege za moja kwa moja kuelekea nchini humo.
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa na wanaharakati wa haki za binadamu wameonya kuwa hatua yoyote ya kuifanya Venezuela kuwa sehemu ya Marekani inaweza kuvunja misingi ya sheria za kimataifa na kuongeza mvutano wa kisiasa duniani.
Zaidi ya mashirika 40 ya haki za binadamu Amerika Kusini yameeleza kuwa licha ya umuhimu wa Venezuela kupata mabadiliko ya kidemokrasia, matumizi ya nguvu au hatua za upande mmoja hayawezi kuhalalishwa.
Kwa mujibu wa sheria za Marekani, Trump hawezi kuifanya Venezuela kuwa jimbo la Marekani bila idhini ya Bunge la Marekani pamoja na ridhaa ya wananchi wa Venezuela wenyewe.