×

Tuzo za Vinywaji ‘Best Brand Beverage’ 2026 Kufanyika Juni 28 Mlimani City, Dar

Taasisi ya Best Brand Africa kwa kushirikiana na Standout Marketing Ltd (EA) imetangaza rasmi kufanyika kwa tuzo za BEST BRAND BEVERAGE 2026, zitakazofanyika Juni 28, 2026 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Masoko, Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa Best Brand Africa, Faithbeth Mkenda, amesema tuzo hizo zinalenga kutambua, kuthamini na kusherehekea ubora wa chapa katika sekta ya vinywaji nchini Tanzania, hususan katika ubunifu, ushindani, huduma na mchango wa kiuchumi.

Amefafanua kuwa hafla hiyo itafanyika katika ukumbi wa Mlimani City Conference Hall na itahusisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo, ambapo jumla ya makampuni 30 yanatarajiwa kushiriki.

Mkenda amesema tuzo hizo zitahusisha makundi yote ya sekta ya vinywaji ikiwemo maji ya kunywa, juisi, soda, vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks), vinywaji vya lishe, vinywaji vya asili na herbal, vinywaji vya maziwa pamoja na vinywaji vya kileo.

Ameongeza kuwa vigezo vitakavyotumika kujadili washindi ni pamoja na masoko, ubora wa chapa, huduma kwa wateja na ubunifu, huku akisisitiza kuwa wamefanya kazi na taasisi husika kuhakikisha viwango na masharti yote yanazingatiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Standout Marketing Ltd (EA), Ramadhan Mbalamwezi, amesema kampuni yao iko tayari kushirikiana kikamilifu kuhakikisha mafanikio ya tukio hilo ambalo linatarajiwa kuwa la kila mwaka.

Amesema tukio hilo litakuwa jukwaa muhimu la kutambua mchango wa makampuni ya vinywaji na kukuza ushindani wa kibiashara ndani na nje ya nchi.

Tuzo za BEST BRAND BEVERAGE 2026 zinatarajiwa kuibua hamasa mpya katika sekta ya vinywaji na kuimarisha ubora wa bidhaa sokoni nchini Tanzania.

Leave a Comment