×

Yanga Yaanza Rasmi Ujenzi wa Uwanja Wake wa Kihistoria – Video

Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Eng. Hersi Ally Said

Uongozi wa klabu ya Young Africans Sports Club (Yanga SC) imetangaza rasmi kuingia katika hatua mpya ya kihistoria ya ujenzi wa uwanja wake binafsi, ndoto ambayo imekuwa ikiota mizizi kwa takribani miaka 90 ya historia ya klabu hiyo.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Mwenyekiti wa klabu hiyo Eng. Hersi Ally Said amesema uongozi na wanachama wa Yanga wanapaswa kujivunia juhudi za viongozi waliopita walioweka msingi imara wa klabu, ikiwemo kuhifadhi ardhi yenye ukubwa wa mita za mraba 35,000 kwa zaidi ya miaka 50, ikiwa ni hazina muhimu ya kufanikisha mradi huo leo.

Amesema kupitia juhudi hizo za muda mrefu, klabu imeweza kufikia hatua ya kuanza rasmi safari ya kujenga uwanja wake wenyewe, hatua inayoonekana kama matokeo ya historia, uzalendo na mshikamano wa Wananchi.

Katika maelezo yake, Eng. Hersi amesema awali alipoingia madarakani, dhamira yake kuu ilikuwa ni kuhakikisha Yanga inapata uwanja wake binafsi. Hata hivyo, alibaini kuwa mafanikio ya kiuchumi na kiushindani ndani ya uwanja wa mchezo yalikuwa muhimu kwanza ili kuvutia wawekezaji.

Ameeleza kuwa baada ya klabu kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali, imeongeza mvuto kwa wawekezaji na kuongeza idadi ya wanachama ndani na nje ya nchi, hali iliyosaidia kufungua milango ya uwekezaji mkubwa.

Yanga SC ilipotangaza zabuni ya ujenzi wa uwanja huo, kampuni mbalimbali zilijitokeza kuonyesha nia ya kushiriki katika mradi huo mkubwa. Baada ya mchakato wa tathmini, Kamati Kuu ya klabu iliidhinisha GSM Group kuwa mbia mkuu wa ujenzi wa uwanja huo wa kisasa.

Eng. Hersi ametangaza rasmi kuwa Yanga SC na GSM Group wameingia katika makubaliano ya ubia wa umiliki wa uwanja kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50.

Ameongeza kuwa klabu itatoa ardhi kwa ajili ya mradi huo, huku GSM Group ikichangia uwekezaji mkubwa wa kifedha utakaosaidia ujenzi wa uwanja wa kisasa unaotarajiwa kubadili historia ya klabu hiyo.

Kwa mujibu wa uongozi, ujenzi wa uwanja huo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 18 hadi 20, na uzinduzi wake rasmi unatarajiwa kuwa sehemu ya historia mpya ya Yanga SC.

Uongozi umetoa shukrani kwa Ghalib Said Mohamed na familia yake kwa mchango wao mkubwa na uamuzi wa kushiriki katika mradi huo, hatua inayoonekana kama mfano wa uwekezaji wa kizalendo wenye lengo la kuendeleza michezo nchini.

Mradi huo unatajwa kuwa moja ya miradi mikubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo, ukiwa na matarajio ya kuimarisha hadhi ya Yanga SC ndani na nje ya Tanzania.

Leave a Comment