
Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Airtel Tanzania na kampuni ya teknolojia ya Huawei zimethibitisha upya dhamira yao ya kuendelea kuimarisha huduma za mawasiliano nchini kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa na ubunifu vilivyojadiliwa katika Kongamano la Huawei Mini Mobile World Congress (Mini MWC).
Kampuni hizo zimesema ushirikiano wao unaendelea kulenga kuharakisha mageuzi ya kidijitali, kupanua huduma za mtandao na kuboresha uzoefu wa wateja kupitia suluhisho za kisasa za mawasiliano.
Akizungumza wakati wa kongamano hilo lililofanyika Tanzania Mei 12, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alisema ushirikiano huo unaendelea kuwa sehemu muhimu katika kusaidia ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
“Ni furaha kubwa kushiriki nanyi leo tunapojadili mustakabali wa sekta ya mawasiliano, mageuzi ya kidijitali na fursa zinazoendelea kujitokeza ndani ya soko letu na ukanda mzima,” alisema.
Mkutano huo uliwakutanisha viongozi na wataalamu wa kiufundi kutoka kampuni zote mbili kujadili teknolojia za baadaye zinazolenga kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini Tanzania.
Miongoni mwa maeneo ya kimkakati yaliyojadiliwa ni pamoja na ukuaji wa huduma za intaneti ya simu na majumbani, matumizi ya mitandao msingi inayotumia Akili Unde (AI), maendeleo ya teknolojia ya microwave pamoja na mifumo ya kisasa ya usafirishaji wa taarifa kwa njia ya kidijitali.
Kupitia ushirikiano huo, Airtel Tanzania na Huawei pia walijadili matumizi ya teknolojia za kisasa za wireless na AI zinazolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za mtandao, kuboresha uthabiti wa huduma, kuongeza uzoefu wa wateja na kupunguza matumizi ya nishati katika mifumo ya mawasiliano.
Kamoto alisema matumizi ya teknolojia za kizazi kijacho yataongeza matumizi ya data, kusaidia ukuaji endelevu wa biashara na kuiweka Airtel katika nafasi ya kuwa kampuni kinara wa mawasiliano ya kidijitali nchini.
“Tunaendelea kuwa na malengo makubwa na dhamira thabiti katika kusukuma mbele dira ya Airtel kupitia ubunifu na ujumuishaji,” alisema.
Kwa upande wake, Huawei ilisema ushirikiano wake na Airtel Tanzania utaendelea kuwa nguzo muhimu katika safari ya mageuzi ya kidijitali nchini Tanzania.
Kampuni hiyo pia iliipongeza menejimenti ya Airtel Tanzania kwa kushiriki katika majadiliano ya kimkakati yanayolenga kukuza sekta ya mawasiliano nchini na kuhamasisha matumizi ya teknolojia mpya zinazoibukia.
Mini MWC ni jukwaa maalum linaloandaliwa na Huawei Tanzania kwa ajili ya kuwapa wadau fursa ya kujionea teknolojia bunifu zinazooneshwa katika Kongamano la Kimataifa la Mobile World Congress linalofanyika kila mwaka mjini Barcelona, Hispania.
Jukwaa hilo pia linawawezesha wadau wa sekta ya mawasiliano kujadili mwenendo wa teknolojia mpya pamoja na matumizi yanayoongezeka ya Akili Unde (AI) katika kuboresha huduma za mawasiliano nchini.
Baadhi ya viongozi wa Huawei waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na Rais wa Idara ya Bharti Group Key Account, Jack Huang, pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mauzo wa Huawei Tanzania, Galving Gao.
Kongamano hilo limefanyika wakati ambapo sekta ya mawasiliano nchini Tanzania inaendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa huduma za intaneti, matumizi ya huduma za kidijitali na ongezeko la matumizi ya data kutokana na mahitaji yanayoongezeka ya huduma bora na nafuu za mtandao.