
Sakata linalomhusu Spika wa zamani wa Bunge la Uganda, Anita Among, limeendelea kuibua mjadala mkubwa nchini humo baada ya vyombo vya usalama kuanzisha uchunguzi dhidi yake kuhusu madai ya utajiri usioelezeka, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na tuhuma za utakatishaji fedha.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali kutoka Uganda, maafisa wa upelelezi waliinasa baadhi ya mali zinazodaiwa kuhusishwa na Among, ikiwemo gari la kifahari aina ya Rolls-Royce Cullinan lenye thamani ya mabilioni ya shilingi za Uganda, pamoja na nyaraka, simu, fedha za kigeni na vifaa vya kielektroniki vilivyokuwa katika makazi yake jijini Kampala na eneo la Kigo.

Taarifa hizo zimezidi kuongeza mjadala mkubwa kuhusu maisha ya kifahari ya viongozi wa umma nchini Uganda, huku wananchi na baadhi ya wanasiasa wa upinzani wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu chanzo cha mali hizo.
Wakati huo huo, Kamanda wa Jeshi la Uganda na mwenyekiti wa Patriotic League of Uganda (PLU), Muhoozi Kainerugaba, alitangaza kuondoa rasmi uungwaji mkono wake kwa Anita Among katika kinyang’anyiro cha uspika wa Bunge la 12 la Uganda.
Kupitia taarifa iliyotolewa na chama chake cha PLU, Muhoozi aliwataka wabunge kusubiri maelekezo ya Rais Yoweri Museveni kuhusu mgombea rasmi wa uspika.
Aidha, Muhoozi aliandika kwenye mtandao wa X kuwa tayari wamekwishaamua Spika mpya wa Bunge na kwamba “atakayekuwa Spika ni mwanaume,” kauli iliyotafsiriwa na wengi kama ishara ya kupungua kwa nguvu ya kisiasa ya Anita Among ndani ya chama tawala.
Licha ya sakata hilo kuendelea kushika kasi, Anita Among bado hajatoa tamko rasmi lenye maelezo ya kina kuhusu uchunguzi unaoendelea dhidi yake, huku mamlaka za Uganda zikisema uchunguzi bado unaendelea.